Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Maendeleo ya Vijana ni Kipaumbele cha Rais Samia: Katambi


Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya maendeleo ya vijana nchini.

Aidha, Mhe. Katambi amesema vijana ni nguvu kazi ya taifa, hivyo kuwezesha kundi hilo kunatoa fursa kubwa ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuwafanya vijana kuwa chachu kwa maendeleo ya nchi.

Ameyasema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Programu ya Mpango wa Ulinzi wa Vijana Awamu ya Pili “Safeguard Young People (SYP)” iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Vile vile, Naibu Waziri Katambi amesema serikali imeboresha mwongozo wa utoaji mikopo kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana ambapo kwa sasa mfuko huo unatoa mikopo kwa kijana mmoja mmoja, ambapo maboresho hayo yatawawezesha vijana walio katika sekta isiyo rasmi na wahitimu wa vyuo kujiajiri kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali.

Kwa upande wengine, Mhe. Katambi amesema programu ya Safeguard Young People ni fursa kwa vijana kujikwamua na changamoto za kijamii na kiuchumi, hivyo amehamasisha ushirikiano katika utekelezaji wa programu hiyo ili kufikia malengo na kuleta mabadiliko chanya kwa vijana.

Naye, Balozi wa Switzerland Nchini Tanzania, Mhe. Didier Chassot amesema serikali ya Uswisi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza programu hiyo ya SYP kwa lengo la kuwaondolea vijana changamoto za kiafya, kiuchumi, kisaikolojia na kijamii.

Programu ya Mpango wa Ulinzi wa Vijana “Safeguard Young People (SYP)” inalenga kuboresha huduma za afya, elimu ya afya kwa vijana, kuongeza ushirikishwaji wa vijana katika ngazi za maamuzi na pia kuwaunganisha vijana na fursa za kujipatia ujuzi na kipato.