Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

MAKATIBU WAKUU WATEMBELEA KIWANDA CHA KILIMANJARO KUJIONEA ZOEZI LA USIMIKAJI MITAMBO


Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Andrew Massawe akifafanua jambo wakati alipotembelea Kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro kujionea tukio la usimikwaji wa mitambo (Machines) katika Kiwanda hicho kilichopo Moshi, Mkoani Kilimanjaro.


*Waahidi kuhakikisha kiwanda kinapata malighafi bora na masoko

*PSSSF itaendelea kutimiza wajibu wake

Makatibu wakuu kutoka katika wizara nne wametembelea na kujionea tukio la usimikwaji wa mitambo (Machines) katika Kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro (KILCL) likiendelea kwa kasi na kutoa wito kiwanda hicho kianze kazi ya uzalishaji mapema kama ilivyopangwa.

Makatibu Wakuu waliokuwa katika ziara hiyo ya kikazi ni pamoja na; Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bw. Andrew Massawe, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Bw. Christopher Kadio na Naibu katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Ludovick J. Nduhiye.

Baadhi ya wataalamu kutoka Kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Viwanda na Biashara wakifuatilia kwa makini maelezo ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Andrew Massawe

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Andrew Massawe ambaye ndiye alikuwa mwenyeji wa ziara hiyo, alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ya Makatibu Wakuu wa Wizara hizo za kisekta ambazo zinahusika moja kwa moja zitasaidia katika ukuaji wa kiwanda hiko, hivyo ili kiweze kuendelea kama ilivyokusudiwa.

“Nimeona niwakaribishe Makatibu Wakuu kutoka kwenye Wizara zinazohusika katika mchakato mzima wa kiwanda hiki ili kila mmoja aweze kujionea hatua iliyofikiwa na kutoa michango yao katika ambayo itasaidia kiwanda hiki kuzalisha bidhaa bora zitakazo pata soko ndani na nje ya nchi,” alisema Massawe

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifungo na Uvuvi (Mifungo), Prof. Elisante Ole Gabriel akieleza jambo wakati wa ziara hiyo.

Aliongeza kuwa, hapo awali kulikuwa na changamoto ya malighafi akitolea mfano wa hali ya ubora wa ngozi, hivyo Katibu Mkuu wa Mifugo amekuja huku akiwa ameambatana na timu ya wataalam wake ili suala hilo lipatiwe ufumbuzi.

Sambamba na hayo alielezea changamoto ya masoko ambayo imepelekea kwa baadhi ya taasisi hapa nchini kutokununua bidhaa zetu, katika kutafuta ufumbuzi wa saula hilo Wizara ya Viwanda na Biashara itasaidia suala zima la ukuzaji masoko ya bidhaa zitakazozalishwa kiwandani hapo.

Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro Bw. Masoud Omari akifafanua jambo kwa Makatibu Wakuu kuhusu zoezi la usimikaji wa Mitambo

Katika ziara hiyo, Makatibu Wakuu wote walitoa ahadi ya kushirikiana kwa pamoja kwa lengo la kuhakikisha kiwanda hicho cha bidhaa za ngozi kinazalisha bidhaa zenye ubora na ambazo zinatapata soko la ndani na nje.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Bw. Masoud Omari alisema ujenzi wa awamu ya kwanza umshakamilika na ufungaji wa mitambo kiwandani hapo unaendelea na hatua hiyo itakapo kamilika shughuli za uzalishaji katika kiwanda hicho itaanza hivi karibuni.

“Awamu ya pili ya ujenzi inahusisha kiwanda cha kuchakata ngozi ambacho kimefikia asilimia 20 na kinatarajiwa kukamilika Januari, 2021. Hatua inayoendelea sasa ni usimikwaji wa Mitambo katika majengo yaliyokamilika awamu ya kwanza tunatarajia hadi kufikia mwezi mei, 2021 usimikaji wa mitambo katika majengo ya awamu ya pili utakuwa umekalika na baada ya hapo kiwanda kutaanza uzalishaji” alifafanua Bw. Omari.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Bw. Hosea Kashimba ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya kiwanda cha Kilimanjaro, aliwashukuru makatibu wakuu wote waliotembelea kiwanda hicho na alisema anatarajia kiwanda hicho kitaleta tija iliyokusudiwa kwa wananchi.

“Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma uliamua kuwekeza katika kiwanda hicho ikiwa ni hatua ya kuitikia mwito wa serikali ya awamu ya tano ambayo ilielekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza kwenye viwanda ambavyo vitaleta tija kwa taifa,” alieleza Kashimba