Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Naibu Waziri Kisuo akagua viwanda Pwani


✅ Asisitiza Uwekezaji wenye Tija na Matumizi ya Teknolojia

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo, amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Mkuranga, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Sheria za Kazi katika viwanda pamoja na kutathmini fursa za ajira zinazotokana na uwekezaji wa viwanda nchini.

Katika ziara hiyo aliyoifanya Machi 6, 2026, Mhe. Kisuo alitembelea Kiwanda cha Kedda pamoja na Kiwanda cha Raddy Fiber Manufacturing kinachotengeneza vifaa vya teknolojia kama simu janja na kompyuta mpakato.

Akiwa katika kiwanda hicho, Naibu Waziri alipata fursa ya kuzungumza na uongozi wa kiwanda pamoja na wafanyakazi, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika sekta ya viwanda kama nguzo muhimu ya kuongeza ajira, kukuza ujuzi kwa vijana na kuharakisha maendeleo ya teknolojia nchini.

Sambamba na hayo, Mhe. Kisuo amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi, hususan katika viwanda vya teknolojia ya kisasa. Alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa ndani, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuongeza fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Vilevile, Naibu Waziri Kisuo alitoa wito kwa wawekezaji kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha ajira zinazotokana na uwekezaji huo zinawanufaisha Watanzania huku wakizingatia sheria na taratibu za kazi nchini.

Ziara hiyo imelenga kuhamasisha ukuaji wa sekta ya viwanda kama njia ya kuongeza ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji na kufuatilia mchango wa viwanda hivyo katika kukuza uchumi na ajira kwa Watanzania.