News
Michezo Kazini Chachu ya Afya Bora na Mshikamano Kazini: Kamishna Mkangwa
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Mary Maganga, amesisitiza umuhimu wa michezo kwa wafanyakazi kama njia ya kuimarisha afya, mshikamano na tija kazini.
Kauli hiyo imesemwa kwa niaba yake na Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa, aliyesoma hotuba yake wakati wa kufunga Bonanza la Michezo ya Wafanyakazi katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Veneti, Njombe, leo Aprili 26, 2026, Bi. Maganga amewataka wafanyakazi nchini kuendeleza utamaduni wa kushiriki michezo.
“Utamaduni wa michezo kazini ukiendelezwa tutakuwa na wafanyakazi wenye furaha, ari, na wenye uwezo wa kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” alisema Bi. Mkangwa akinukuu hotuba ya Katibu Mkuu.
Bonanza hilo la siku mbili lilikuwa sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi linaloandaliwa na Wakala wa Afya na Usalama Mahala pa Kazi (OSHA). Katika hotuba hiyo, Kamishna Mkangwa alizitaja faida nne kuu za michezo kazini: kwanza, kuboresha afya ya mwili na akili ya wafanyakazi; pili, kuongeza mshikamano na mahusiano bora kazini; tatu, kupandisha tija na morali ya kazi; na nne, kuchochea ubunifu unaoleta matokeo chanya kwa taasisi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, aliwapongeza wafanyakazi walioshiriki michezo hiyo kwa siku mbili, akisema imechangia moja kwa moja kuimarisha afya zao na kujenga undugu miongoni mwao.
Katika dimba, Ofisi ya Waziri Mkuu ilifanikiwa kupata medali katika michezo ya riadha kwa wanaume na wanawake, pamoja na kushika nafasi ya pili katika mchezo wa kuvuta kamba upande wa wanawake.
Katibu Mkuu Maganga amehitimisha kwa kusisitiza kuwa mabonanza ya michezo yanapaswa kuendelezwa hata baada ya maadhimisho ya Mei Mosi, kama sehemu ya mikakati ya kudumu ya kuboresha ustawi wa wafanyakazi.
