News
Mradi wa Mzizima Towers kukamilika Disemba 2026
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema mradi wa uwekezaji wa jengo la kitega uchumi mzizima towers umefikia asilimia 91 huku akisisitiza wanatarajia kuukamilisha ifikapo Disemba mwaka huu 2026.
Aidha, Mradi huo ambao hadi kukamilika kwake utagharimu Sh. bilioni 322 ambapo mpaka sasa zimetumika Sh. Bilioni 201 ambazo zimeufikisha mradi huo katika asilimia 91.
Waziri huyo amesema hayo tarehe 16 Machi, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Bunge Usatawi na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea na kukagua mradi huo unaotekelezwa kwa asilimia 100 na fedha za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Alisema mradi huo umezingatia viwango vya kisasa vya usanifu, mahitaji ya biashara, makazi, huduma za kitalii, na unahoteli ya hadhi ya nyota tano.
Alisema utakuwa na maeneo ya ofisi za umma, maduka na kumbi za mikutano, sehemu ya kuogelea na kufanyia mazoezi.
Alisema mradi ulianza April 2013, ulitarajia kukamilika Machi 2017 lakini ulisimama kupisha ukaguzi wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) mwaka 2016 ulio fuatiwa na ukaguzi maalumu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuanzia mwaka 2019-2022 serikali ilielekeze shughuli zisimame ufanyike ukaguzi maalumu.
Aidha alisema kingine kilichokwamisha ni masharti ya ujenzi ya hoteli ya kimataifa kwamba inapojengwa lazima awe amepatikana mwekezaji kwahiyo walichelewa kwa sababu ilikuwa lazima wampate kwanza, janga la uviko 19, na kuchelewa kwa mchakato wa kumpata msanifu wa mradi.
“Hata hivyo, changamoto hizo zilitatuliwa na ujenzi unaendelea kazi zinazo endelea ni ukamilishaji wa miundombinu ya maji safi na maji taka, miundombinu ya umeme, upakaji wa rangi, umaliziaji wa kuta, uwekaji wa vioo madirisha na milango.
“Kukamilika kwa mradi kutaongeza mapato ya mfuko kupitia hoteli na ofisi, kuongeza thamani ya mfuko na uwezo wa kulipa mafao kwa wanachama, kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali, kuchochea ajira, kuanganisha sekta ya biashara na utalii katika jiji la Dar es Salaam” alisema waziri huyo
Mradi wa jengo hilo unajumuisha minara miwili ambapo kati ya hiyo kuna wa jengo la biashara lenye ghorofa 35 na wa makazi wenye ghorofa 32. na umezingatia viwango vya kisasa vya usanifu wa majengo ya kitaifa.
Baada ya kusikiliza wasilisho la waziri huyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Hawa Mchafu alisifu maendeleo ya mradi na kushauri ukamilike kwa muda uliopangwa hiyo itasaidia kuleta tija kwa wanachama wao.
“Niwampongeze wanakamati sisi tuatendelea kuwa pamoja nanyi katika mradi huu mpaka pale utakapo tamatika” alisema
