Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Munisi: Amani ya Taifa inajenga kwa Ushirikiano


Naibu Waziri , Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Dkt. Evaline Munisi (Mb), amesema Serikali inaendelea kuthamini na kutambua mchango mkubwa wa viongozi wa dini katika kuimarisha amani, mshikamano, maadili na maridhiano ya kitaifa, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu ya Tanzania.

Kauli hiyo imesemwa wakati akimuakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe.Deus Sangu (Mb) katika Kongamano la Kuliombea Taifa lililoandaliwa na Kanisa la Haki Ministry kwa kushirikiana na Umoja wa Makanisa ya Kitume na Kinabii Tanzania leo Julai 12,2026 Mkoani Morogoro.

Katika salamu zake, Dkt. Munisi alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka mkazo katika kuimarisha umoja wa Watanzania kupitia maridhiano, ushirikiano na ushirikishwaji wa makundi mbalimbali ya kijamii.

Aidha, alisema amani na mshikamano ni msingi wa maendeleo ya Taifa, akiwataka viongozi wa dini kuendelea kutumia nafasi zao kuhubiri upendo, haki, uvumilivu na uzalendo miongoni mwa wananchi. Alinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyesema kuwa “Amani bila haki si amani, na haki bila amani haiwezi kudumu,” akisisitiza kuwa maadili na haki ni msingi wa amani ya kudumu nchini.

Kwa upande wake, Dkt. Nabii Joshua Aram Mwantyala alisema kongamano hilo limewakutanisha zaidi ya viongozi 1,000 wa dini kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuliombea Taifa, viongozi wake na wananchi wote. Alieleza kuwa Kanisa lina wajibu wa kuendelea kuhubiri amani, mshikamano, haki na maadili kwa kuzingatia mafundisho ya Biblia yanayowataka waumini kuwaombea viongozi wenye mamlaka ili Taifa liendelee kuishi katika utulivu na maendeleo.

Dkt. Mwantyala pia aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi zake za kudumisha amani, umoja na maendeleo nchini, huku akimuomba Dkt. Munisi kuufikisha ujumbe wa viongozi wa dini kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuendelea kuwa na ujasiri, hekima na moyo wa kulitumikia Taifa. Alisisitiza kuwa viongozi wa dini wataendelea kuiombea Serikali na wananchi wote ili Tanzania iendelee kuwa mfano wa amani na mshikamano barani Afrika.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiroho wakiwemo mitume, manabii, maaskofu, wachungaji, waalimu na wainjilisti kutoka madhehebu tofauti nchini, likiwa na lengo la kuimarisha mshikamano wa kitaifa kupitia maombi, mafundisho ya kiroho na ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini katika kujenga Taifa lenye amani, haki na maendeleo endelevu.