Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Dkt. Munisi Afungua Mkutano Mkuu wa Tuico


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Dkt. Eveline Munisi amefungua Mkutano Mkuu wa Saba (7) wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) Taifa uliofanyika mkoani Iringa, leo Agosti 5, 2026.

Aidha, Mkutano huo umeambatana sambamba na zoezi la uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Dkt. Munisi amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wafanyakazi katika ujenzi wa uchumi wa Taifa na itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha maslahi yao yanalindwa.

Kadhalika, amewapongeza TUICO kwa mafanikio makubwa tangu kuanzishwa mwaka 1995, ikiwemo kuongezeka kwa wanachama hadi kufikia zaidi ya 150,000.

Vile vile, Dkt. Munisi amesisitiza kuwa uchaguzi wa viongozi wa vyama vya wafanyakazi lazima uendeshwe kwa uwazi, haki na mshikamano. “Chama cha wafanyakazi hakiwezi kuwa imara kama hakuna uwazi, misingi ya haki na kuheshimiana katika mchakato wa kura,” amesema.

Ameongeza kuwa, uwepo wa vyama vya wafanyakazi ni haki ya kikatiba na haitavumilia waajiri wanaokwamisha uanzishwaji wake. Pia, amesisitiza kuhusu utekelezaji wa suala la kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi kusimamia kikamilifu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James amepongeza viongozi na wanachama wa TUICO kwa kuendelea kufanya mabadiliko ya uongozi kwa mujibu wa katiba yake.

Naye, Kaimu Mwenyekiti wa TUICO Taifa, Bw. Abdallah Msese amesema chama kimeendelea kunufaika na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi, kupandisha mafao ya wastaafu, kupandisha watumishi madaraja, kuajiri na kuweka mazingira bora ya kazi.