Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Naibu Waziri Katambi atoa Maagizo kwa Maafisa Maendeleo ya Vijana Nchini


* Ametaka Mikopo inayotolewa na Halmashauri kupitia mapato ya ndani ziwafikie Wananchi.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi ametoa wito kwa Maafisa Vijana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kote nchini kuwa na utaratibu wa kufanya ufuatiliaji katika miradi ya vijana wanufaika wa mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na serikali.

Ameeleza kuwa, mfumo huo wa ufuatiliaji utawawezesha kutambua kwa karibu miradi yenye tija ambayo vijana wamewekeza sambamba na kujua hali ya utekelezaji wa shughuli zao za kujikwamua kiuchumi na kuwaletea maendeleo.

Mheshimiwa Katambi amesema hayo wakati akizungumza na vijana katika ziara yake ya kikazi Mkoani Singida ya kukagua na kufuatilia uratibu wa utekelezaji wa sera na sheria za uwezeshaji vijana na Watu wenye Ulemavu kupitia mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na haki na stahiki za Watu wenye Ulemavu.

Amesema kuwa, Serikali kupitia halmashauri zilizopo nchini imekuwa na wajibu wa kutenga fedha kupitia makusanyo ya mapato ya ndani ambapo mikopo ya asilimia 4 kwa Vijana, 4% Wanawake na 2% Watu wenye Ulemavu imekuwa ikitolewa kwa lengo la kuwawezesha kuanzisha miradi, kuendeleza shughuli zao ambazo zitatoa fursa za ajira na kuwaingizia kipato.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhesimiwa. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwezesha vijana kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu ili wajiajiri na kuajiri vijana wenzao kupitia shughuli za kiuchumi watakazoanzisha,” amesema

Aidha, Naibu Waziri Katambi amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuangalia namna bora ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa za mikopo hiyo na kuwapatia ujuzi ambao utawasaidia kuanzisha miradi yenye tija, kusimamia shughuli zao sambamba na kuwajengea mbinu za kukuza biashara. Pia, amehamasisha halmashauri kuwa na utaratibu wa kukopesha tena vikundi vya vijana, wanawake na wenye Ulemavu ambavyo vinarejesha mikopo hiyo kwa wakati.

Vile vile, amesema katika kuimarisha Uwezeshaji wa vijana kiuchumi kupitia shughuli za Uzalishajimali Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kusimamia na kuhakikisha kila halmashauri inatenga maeneo kwa ajili ya vijana kufanya shughuli zao kiuchumi.

Naye, Mnufaika wa kikundi cha Chapa Kazi, Mwanahamisi ameishukuru serikali chini ya uongozi mahiri wa Mhesimiwa. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua mchango wa vijana katika kusukuma gurudumu la maendeleo, hivyo wameahidi kuchapa kazi kwa bidii na uzalendo ili waweze kurejesha mikopo hiyo kwa wakati na kuwafanya wananchi wengine waweze kunufaika na fursa hiyo.

Mara baada ya ziara hiyo ya kutembeea vikundi vya vijana vilivyonifaika na mikopo inayotolewa na halmashauri pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana katika halmashauri ya Manyoni, Ikungi na Singida Mjini, Naibu Waziri Katambi alitembelea Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu – Sabasaba, Mkoani Singida na kujionea utekelezaji wa mafunzo yanayotolewa kwa vijana 108 wenye Ulemavu. Pia alitembelea vijana wanufaika wa mafunzo ya kilimo cha Kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba (Greenhouse) katika halmashauri ya Ikungi na Ilongelo, Mafunzo hayo yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia programu ya kukuza ujuzi.

MWISHO