News
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Kujadili Hifadhi ya Jamii
Tanzania imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha sekta ya hifadhi ya jamii na ustawi wa wananchi kupitia ushirikiano wa kikanda baada ya viongozi wa sekta za kazi, ajira na maendeleo ya jamii kushiriki kikao cha awali cha maandalizi ya mkutano wa mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kilichofanyika leo Julai 7, 2026, jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kiliongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi ,Ajira na Mahusiano Bi. Mary Maganga aliyeshirikiana na Dkt. Kedmond Mapana Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana na Wakili Amon Mpanju Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambapo walipitisha ushiriki wa mawaziri wa Tanzania kuelekea kikao cha pamoja cha kikanda.
Bi. Maganga alieleza kuwa majadiliano hayo ni sehemu ya maandalizi ya kikao cha mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kitakachowakutanisha wawakilishi kutoka Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan Kusini, Somalia na Burundi kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuboresha mifumo ya hifadhi ya jamii kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika kikao hicho Mawaziri watakaoiwakilisha Tanzania katika majadiliano hayo ni Mhe. Dkt. Joel Nanauka, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana , Dkt. Eveline Munisi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano pamoja na Mhe. Maryprisca Mahundi Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambao walishiriki kikao cha maandalizi.
Imeelezwa kuwa miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa ni kazi na ajira, hifadhi ya jamii, maendeleo ya vijana, jinsia na wanawake, ustawi wa watoto pamoja na masuala ya uhamiaji.

