Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Ofisi ya Waziri Mkuu yasherekea Idd na wanafunzi wenye ulemavu


Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa chakula cha mchana na kushiriki pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo ambacho ni maalum kwa watu wenye ulemavu katika kusherekea sikukuu ya Eid El Fitr.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, amesema lengo la kuandaa chakula hicho ni kuendeleza umoja na kutoa faraja kwa kundi hilo la watu wenye ulemavu.

“Katika kusherekea sikukuu hii ya Eid El Fitir, Ofisi ya Waziri Mkuu iliona ni muhimu kuandaa chakula cha mchana na kushiriki pamoja na vijana wetu wa chuo hiki cha watu wenye ulemavu hivyo Waziri Mkuu pamoja na Waziri wetu wa Nchi, Mhe. Jenista Mhagama wamenituma niwawakilishe katika tukio hili kwasababu wao wapo katika majukumu mengine ya kitaifa,” amesema Ummy Nderiananga.

Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo, Prof. Jamal Katundu, ametoa wito kwa taasisi na watu binafsi kujenga utamaduni wa kuyajali na kuyasaidia makundi mbali mbali ya watu wenye mahitaji maalum kikiwemo chuo hicho cha watu wenye ulemavu.

“Hili jambo kubwa sana na ndiyo maana mimi kama Naibu Katibu Mkuu nimepewa jukuma la kuratibu suala hili na kama mlivyoona vijana wetu wamefurahishwa sana na tukio hili hivyo natumie fursa hii kutoa wito kwa watu wenye uwezo na taasisi mbali mbali zenye mafungu ya kusaidia jamii kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kuja kuwasaidia vijana wetu,” Prof. Jamal Katundu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa, amesema menejimenti pamoja na wanachuo wamelipokea tukio hilo kwa furaha sana ambapo ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa tukio hilo.

Aidha, baadhi ya wanachuo wakiwemo Joseph Baraza na Evodia Mwombeki wameelezwa kufurahishwa na tukio hilo na wameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na viongozi mbali mbali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambao walijumuika nao katika chakula hicho.

“Tumefurahi sana kwa namna moja ama nyingine kwasababu huwa tunajisikia furaha sana kujumuika na watu tofauti tofauti na kujiona kwamba hatujatengwa,tunawashukuru sana kwa tukio hili la leo na Mungu awabariki sana,” amesema Evodia Mwombeki, Mwanafunzi katika fani ya Kilimo na Ufugaji.

Chuo cha Ufundi Stadi Yombo cha watu wenye ulemavu ambacho kipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kilianzishwa mwaka 1973 kwa malengo ya kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu nchini. Kwasasa kina jumla ya wanafunzi 76 na kinatoa kozi mbali mbali zikiwemo; Ufundi Umeme, Uwashi, Ushonaji, Uchomeleaji Vyuma pamoja na Kilimo na Ufugaji.