Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Waziri Sangu Amtembelea Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, Februari 12, 2026 amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, nyumbani kwake Jijini Dodoma.

Ziara hiyo imelenga kupata uzoefu na ushauri kuhusu ujenzi na uimarishaji wa mahusiano katika jamii, kufuatia kuanzishwa kwa Kitengo cha Mahusiano na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuimarisha mshikamano na kuwa na mwelekeo mmoja katika sekta za kidini, kiraia na nyinginezo.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Mhe. Sangu amesema tayari wameanza mchakato wa kukutana na viongozi wa dini mbalimbali wakiwemo The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT), Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) na Kanisa la Waadventista wa Sabato.

Mhe. Sangu amempongeza Mhe. Pinda kwa mchango wake katika kuasisiwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano na Amani ya Viongozi wa Dini, akieleza kuwa uzoefu wake katika masuala ya migogoro ya kijamii ni hazina muhimu katika kuimarisha sekta ya mahusiano nchini.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, amesema mahusiano ni mchakato unaojengwa kwa misingi ya mazungumzo na uelewano, akisisitiza umuhimu wa kuwa na lugha moja ndani ya jamii ili kudumisha amani na umoja wa Taifa.

Aidha, amempongeza Mhe. Sangu kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kusimamia Sekta ya Mahusiano na kumtaka kuendeleza mahusiano bora na wananchi pamoja na wadau wote wanaomzunguka.

“Mahusiano ni msingi muhimu katika ujenzi wa maendeleo ya Taifa letu,” amesisitiza Mhe. Mizengo Pinda.