Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ndalichako ampongeza Mhe. Rais Samia kwa kufungua fursa za Uwekezaji nchini


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufungua fursa mbalimbali zikiwemo za uwekezaji hapa nchini.

Mhe. Profesa Ndalichako amesema hayo leo tarehe 22 Oktoba, 2022 jijini Dar es Salaam, wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa jengo la kitega uchumi la _Mzizima Tower_ linalomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

“Tunafahamu namna ambavyo Mhe. Rais wetu Samia Suluhu Hassan anafungua fursa za Uwekezaji, kwa hiyo nanyie NSSF mnatengeneza mazingira ambayo wawekezaji watakapokuja nchini watapata sehemu ya kuishi na sehemu ya kufanya biashara zao,” amesema Mhe.Profesa Ndalichako.

Mhe. Profesa Ndalichako amesema kupitia uwekezaji huo wa mradi wa _Mzizima Tower_ inadhihirisha kuwa NSSF inaunga mkono juhudi ambazo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaendana na kazi kubwa ambayo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa anaifanya ya kufungua uchumi wa nchi, kuweka mazingira mazuri kwenye sekta binafsi na kukaribisha wawekezaji nchini.

“Tumeshuhudia kazi kubwa inayofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambavyo imefungua fursa na hivi sasa wawekezaji kutoka Mataifa mbalimbali wanakuja nchini, hivyo bado tunahitaji majengo mengi zaidi ya biashara ikiwemo hoteli ya namna hii,” amesema.

Amewasihi NSSF kuendelea kufanya kazi kwa wakati ili Serikali iweze kuona manufaa ya mradi huu, pia na fedha za wanachama ambazo zimewekezwa kupitia mradi huu zianze kurejeshwa, lakini kubwa zaidi mtengeneze ajira kwa vijana ambapo mradi huo ukianza kufanya kazi ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zinaweza kufika 1000.

Mhe. Profesa Ndalichako pia amepongeza Bodi ya Wadhamini, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba na Managementi kwa kazi kubwa mnayofanya hasa ya kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zimejitokeza katika mradi huu.