Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Rais Samia aahidi kuimarisha maslahi ya Wafanyakazi


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuimarisha maslahi ya wafanyakazi nchini.

Rais Samia ametoa ahadi hiyo wakati akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi kwenye uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma.

Rais Samia amesema kwa kuwa alishatoa ahadi mwaka jana, ameagiza kufanyika kwa majadiliano ya kuimarisha maslahi ya wafanyakazi yanayoendelea kati ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Serikali ili kujua kiwango cha maslahi itakayohitajika.

“Yale tuliyoyafanya mwaka huu, mambo mbalimbali, kupunguza kodi…tutaendelea kuyafanya. Lakini pamoja na hayo, lile jambo letu lipo. Ndugu zangu, jambo letu lipo si kwa kiwango kilichosemwa na TUCTA kwasababu mnajua hali ya uchumi wetu, na hali ya uchumi wa dunia. Hali si nzuri sana, uchumi wetu ulishuka chini mno.”

Kwa upande mwingine, Rais Samia ameagiza Maafisa Rasilimali Watu pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kushughulikia haki na stahiki za watumishi wanaotarajia kustaafu ndani ya miezi sita ili mtumishi anapofika muda wa kustaafu, mafao yake yawe tayari.

Kuhusu watumishi waliofanya kazi kwa muda mrefu na kisha kufukuzwa kazi kwa sababu ya vyeti vya kughushi bila kulipwa malipo yoyote, Rais Samia pia ameagiza Wizara ya Fedha na Mipango kushugulikia stahiki zao zinazotokana na makato ya mishahara yao na kuwalipa.

Rais Samia amesema Serikali imeshaunda Bodi za Kima cha Chini cha Mshahara kwa Sekta Binafsi na ya Umma na tayari zimeshaanza kufanya tathmini ya mishahara iliopo sasa.

Serikali imeendelea kustawisha maslahi ya wafanyakazi tangu mwaka 2021 ikiwemo kupunguza makato ya kodi, kuongeza umri wa wategemezi kutoka miaka 18 hadi miaka 21, kupandishwa vyeo vya watumishi, kubadilisha kada, kulipa malimbikizo ya watumishi pamoja na kutoa ajira mpya.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kustawisha Maslahi ya Wafanayakazi nchini.

"Furaha na bashasha ambazo wafanyakazi wameonyesha ni ishara kuwa wafanayakazi wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kulijenga Taifa na kuwaletea Wananchi Maendeleo,"