Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Sangu ahimiza Diaspora kuchangia kikamilifu maendeleo ya Taifa


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu, amewahimiza Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kuitambua na kuielewa kwa kina Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili waweze kubaini fursa zilizopo na kuchangia kikamilifu maendeleo ya Taifa.

Amesema Dira hiyo inaeleza mwelekeo wa Taifa ambalo Tanzania inalenga kujenga, hivyo ni muhimu kwa Diaspora kuitumia kama mwongozo wa kutambua na kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta za uwekezaji, ajira, ujuzi, ubunifu na matumizi ya teknolojia, kwa lengo la kukuza uchumi na kuongeza Pato la Taifa.

Mhe. Sangu ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Saudi Arabia, ambapo pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Kazi Duniani (Global Labour Market Conference) unaojadili masuala ya soko la ajira duniani.

Katika ziara hiyo, Waziri Sangu pia amekutana na Watanzania wanaoishi na kufanya kazi nchini Saudi Arabia tarehe 24 Januari, 2026, kwa lengo la kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kusikiliza changamoto pamoja na fursa zilizopo kwa Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi.

Alieleza kuwa, Serikali inatambua mchango mkubwa wa Diaspora katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia fedha wanazozituma nyumbani (remittances), uwekezaji, pamoja na kuhamasisha maarifa na ujuzi walioupata nje ya nchi.

Aidha, Waziri Sangu amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi wanalindwa, wanaheshimiwa na wananufaika ipasavyo na fursa za ajira za kimataifa.

Kadhalika, amewahakikishia Diaspora kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira itaendelea kuratibu na kusimamia fursa za ajira kwa Watanzania ili kuhakikisha zinakuwa za staha, salama na zenye haki.

Kwa upande mwingine, Waziri Sangu amesema Serikali kupitia Mfuko wa NSSF imeanzisha mafao yatakayowawezesha Watanzania walioajiriwa katika sekta binafsi pamoja na waliojiajiri kunufaika na huduma za Kinga ya Jamii.