Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Sangu Ateta na Viongozi Bodi ya Wadhamini Kanisa Wadventista Wasabato


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Wadventista Wasabato Taifa katika Ofisi zao jijini Dar es Salaam, Januari 22, 2026.

Katika kikao hicho, Mhe. Sangu aliwapongeza viongozi wa hilo kwa mchango wao mkubwa katika kulinda na kuimarisha amani, mshikamano na maadili mema katika jamii.

Alisema kuwa kanisa hilo limekuwa mstari wa mbele katika kuhubiri maadili mema, uvumilivu na upendo, ambayo ni nguzo muhimu katika kudumisha amani na utulivu wa Taifa.

Aidha, Sangu aliahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Kanisa la Wasabato pamoja na taasisi nyingine za kidini katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya kijamii, ikiwemo elimu, afya na ustawi wa jamii kwa ujumla.

“Ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kidini ni muhimu katika kujenga Taifa lenye maadili, haki na maendeleo endelevu” amesema.

Kwa upande wao, viongozi wa Kanisa la Wasabato wakiongozwa na Mchungaji Joseph Mngwabi, Mwenyekiti wa Union ya Kusini mwa Tanzania, wameishukuru serikali na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika kulinda amani, kuhamasisha maadili mema na kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, wameipongeza serikali kwa juhudi zake zinazoendelea za kuimarisha ajira, kuboresha mazingira ya kazi, na kutumia ajira kama nyenzo muhimu ya kupunguza wigo wa umaskini na kuinua ustawi wa wananchi.