Habari

SERA MPYA YA MAENDELEO YA VIJANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA VIJANA

SERA MPYA YA MAENDELEO YA VIJANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA VIJANA

Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 itakayofanyiwa marekebisho hivi karibuni inategemewa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana hasa katika jitihada za kuwawezesha kujitegemea.

Hayo yamezungumzwa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri , Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana na Ajira,Anthony Mavunde alipokuwa akifungua majadiliano ya wadau wa vijana juu ya Rasimu ya Sera Mpya ya Maendeleo ya Vijana.

Mavunde amesema kuwa maendeleo na ustawi wa vijana nchini ni jambo la muhimu hivyo lazima kuwe na Sera bora inayotoa muongozo kwa ajili ya utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya vijana.

“Sera hii itatoa dira yenye muelekeo wa kuhakikisha Taifa linakua na vijana wenye nguvu, uwezo na ari ya kushiriki katika nyanja za kimaendeleo zitazokuza uchumi wa nchi hivyo wajibu mkubwa wa Serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa kuandaa sera shirikishi, mikakati inayotekelezeka na sheria ambayo ni rafiki kwa maendeleo ya vijana”, alisema Mavunde.

Mavunde ameongeza kuwa Sera hiyo itajenga msingi mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya mwaka 2020 hadi 2025 ambapo malengo yake makubwa ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia viwanda ikiwa ni falsafa inayosisitizwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Amefafanua kuwa hakuna nchi yoyote Duniani ambayo itaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo kama haitawekeza kwenye kundi kubwa la vijana na ndio maana Serikali imeona umuhimu wa kupitia upya sera hiyo kulingana na matakwa ya Dunia.


Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Andrew Massawe amesema kuwa lengo la kufanya mkutano huo ni kuwawezesha wadau wa maendeleo ya vijana nchini kutoa maoni ya pamoja na mkakati wa utekelezaji wa sera hiyo.

“Sera hiyo mpya itawasaidia vijana kwenda sambamba na mabadiliko mbalimbali yanayotokea yakiwemo ya kisera na kijamii ili waweze kuendana na ulimwengu wa sayansi na teknolojia”, alisema Massawe.

Zoezi hilo la ukusanyaji maoni juu ya urekebishaji wa sera hiyo ulianza tangu mwaka 2015 ambapo wadau mbalimbali nchini wakiwemo wa Asasi za ndani na za kimataifa,Wizara na Taasisi mbalimbali, Vyama vya Siasa na Viongozi wa dini.