News
Serikali Yaendelea Kukuza Ajira kwa Wahitimu Kupitia Miradi ya Kimkakati
Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha wahitimu wa vyuo wanapata fursa za Ajira kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati, uendelezaji wa viwanda vidogo na vya kati pamoja na programu za ubunifu nchini.
Kupitia miradi hiyo, zaidi ya Ajira 35,000 zimezalishwa katika ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), huku zaidi ya ajira 10,000 zikitokana na mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Aidha, miradi mingine ya kimkakati iliyochangia upatikanaji wa ajira ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Julius Nyerere ambapo zaidi ya ajira 10,000 zimezalishwa; ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato jijini Dodoma uliotoa zaidi ya ajira 1,500; ujenzi wa Daraja la JPM (Kigongo–Busisi) uliotoa zaidi ya ajira 1,500; pamoja na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam uliozalisha zaidi ya ajira 3,000.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo, Januari 30, 2026, Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Dkt. Regina Christopher Malima (Mbunge wa Viti Maalum) lililouliza kuhusu mikakati ya Serikali katika kuongeza ajira kwa wahitimu wa vyuo kupitia miradi ya kimkakati, viwanda vidogo na vya kati pamoja na programu za ubunifu.
Akijibu swali hilo, Mhe. Kisuo amesema Serikali imetoa mafunzo ya uzoefu wa kazi (Internship) kwa wahitimu 29,902 wa ngazi mbalimbali za elimu, sambamba na kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi 19,075 katika sekta za hoteli, madini, usafirishaji, kilimo na usindikaji wa mazao ya kilimo kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi.
Ameongeza kuwa Serikali imeandaa Mwongozo wa Taifa wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahitimu unaolenga kuweka utaratibu wa utoaji wa mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu, ambao unatumika kwa waajiri wote katika sekta ya umma na binafsi, ili kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
