News
Waziri Sangu azindua baraza la tatu la wafanyakazi PSSSF
✅ Amepongeza Mafanikio ya Mfuko wa PSSSF
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu, amezindua Baraza la Tatu la Wafanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha Mkoani Pwani.
Aidha, Mhe. Sangu amewataka wajumbe wa baraza hilo kuhakikisha wanasimamia vyema yale yote ambayo wafanyakazi wanapaswa kuyafanya kwenye maeneo yao ya kazi ili kuleta ufanisi wa huduma zinazotolewa na kuujenga mfuko kwa lengo la kulinda maslahi ya wanachama na watumishi.
“Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu katika kuimarisha ushirikiano, uwajibikaji na ustawi wa watumishi na hivyo kuchangia ufanisi wa mfuko huu na kuendelea kukuza maendeleo ya sekta ya hifadhi ya jamii nchini,” amesema
Waziri Sangu amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Baraza hilo la wafanyakazi wa PSSSF ambapo amewataka watumishi wa Mfuko huo kujipanga kwa kuanza safari ya utekelezaji wa Dira ya Taifa Maendeleo ya mwaka 2050 Julai mwaka huu.
“Jambo kubwa lililoelekezwa kwenye Dira 2050 ni kukuza uchumi na kuzalisha ajira, tuhakikishe fedha tunazowekeza ziweze kuchochea ukuaji wa uchumi na pili iwe ni miradi ambayo inaweza kuzalisha ajira kwa vijana,” amesema Waziri Sangu.
Kwa upande mwengine, Mhe. Sangu amepongeza uongozi na watumishi wa PSSSF kwa mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo kusajili wanachama wapya ambao wamekuwa wakiajiriwa katika sekta mbalimbali, kukusanya michango, kuboresha utoaji wa mafao kwa wanachama, kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati yenye tija na ambayo inatoa fursa za ajira kwa vijana pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya kidijitali.
Kadhalika, ametoa wito kwa waajiri wa Taasisi za Umma na Sekta binafsi kuhakikisha wanayapatia nafasi mabaraza ya wafanyakazi kwa kuwa yanasaidia ustawi wa wafanyakazi na kuongeza tija katika maeneo ya kazi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Fortunatus Magambo amesema kukutana kwa Baraza hilo ni utekelezaji wa takwa la kisheria ambalo, tangu PSSSF ilipoanzishwa 2018 imekuwa ikizingatia takwa la kisheria kikamilifu.
