Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Serikali na WLF zashirikiana kuimarisha uwezeshaji wa Wanawake na Vijana


Serikali imedhamiria kuimarisha ushirikiano na Jukwaa la Wanawake Viongozi Tanzania (WLF) katika kuharakisha uwezeshaji wa wanawake na vijana nchini.

Juni 1, 2026 jijini Dodoma, Naibu Waziri Dkt. Eveline Munisi alifanya kikao kazi na uongozi wa WLF kujadili maeneo ya kimkakati ya ushirikiano kwenye sekta ya kazi, ajira na mahusiano.

Katika kikao hicho pande hizo mbili ziliafikiana kuwa na maazimio muhimu matatu ambayo ni kuandaa mwongozo wa ushirikiano utakaoainisha maeneo mahsusi ya WLF kuunga mkono vipaumbele vya Serikali.

Pili kuwezesha programu za pamoja za elimu, uhamasishaji na mafunzo kwa wanawake na vijana na tatu kutanua mtandao wa wadau kwa kuiunganisha WLF na taasisi na idara chini ya Wizara kuelekea uzinduzi wa jukwaa hilo.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Munisi aliipongeza WLF kwa kujitambulisha rasmi Serikalini na kuonesha dhamira ya kushirikiana.

“Nawapongeza kwa kuiamini Serikali. Jukumu la kujenga mahusiano bora ni letu sote,” alisema Dkt. Munisi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa WLF, Bi. Chumu Juma Abdallah, alisisitiza kuwa jukwaa hilo linalenga kuongeza thamani katika juhudi za Serikali kupitia uzoefu, ushawishi na mtandao mpana wa wanawake viongozi.

“Kupitia mwongozo wa Serikali, tutakuwa jukwaa muhimu la kujenga wanawake wanaofanya kazi kwa tija, kuongoza kwa busara na kuchangia maendeleo ya Taifa,” alisema Bi. Chumu.

WLF imeeleza nia ya kutambuliwa kama mshirika wa kimkakati wa Serikali katika utoaji wa elimu, majadiliano na programu za kuwawezesha wanawake na vijana.

Mwisho.