Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Sangu aitaka TALGWU kujenga umoja kupitia uchaguzi


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu (Mb.), amekitaka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kuendesha uchaguzi wake kwa kuzingatia Katiba, demokrasia, uwazi, haki, usawa na amani.

Mhe. Sangu ameyasema hayo, Septemba 17, 2026, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa TALGWU katika Ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma, akisisitiza kuwa uchaguzi huo uwe fursa ya kuimarisha umoja na mshikamano badala ya kuwa chanzo cha mgawanyiko.

Amesema Serikali inatambua na kuheshimu uhuru wa vyama vya wafanyakazi na itaendelea kushirikiana navyo kupitia mfumo wa majadiliano ya pamoja katika kushughulikia changamoto na masuala ya maslahi ya wafanyakazi.

“Uchaguzi usiwe chanzo cha mgawanyiko, bali uwe fursa ya kuimarisha umoja na mshikamano. Baada ya matokeo kutangazwa, viongozi na wanachama wote wanapaswa kuendelea kushirikiana, kwa kutambua kwamba TALGWU ni kubwa kuliko mtu mmoja,” amesema Mhe. Sangu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TALGWU Taifa, Ndugu Tumaini Peter Nyamhokya, amesema viongozi wa Chama hicho wamejipanga kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na utulivu, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na TUCTA.

“Tunaishukuru Ofisi yako jinsi ilivyosimama nasi kwenye chaguzi za mikoa zikamalizika salama na kwa amani. Basi na huu wa Taifa pia, nikuhakikishie Mhe. Sangu, utamalizika vizuri,” amesema Ndugu Nyamhokya.