Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Waziri Sangu: Vijana ni nguzo muhimu ya amani


Asema vijana wana nafasi muhimu katika maendeleo ya Taifa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu, amewataka vijana kushiriki kikamilifu katika kulinda amani na usalama kwa kuwa ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.

Ameyasema hayo Septemba 18, 2026, wakati akifungua Jukwaa la 3 la Kitaifa la Ajenda ya Vijana, Amani na Usalama katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Amesema jukwaa hilo ni fursa kwa vijana na wadau kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhisho, huku akieleza kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuzingatia amani, usalama, utawala bora na maendeleo endelevu.

Mhe. Sangu amesema Serikali imeendelea kuwapa vijana nafasi katika masuala ya utawala bora, amani na usalama, sambamba na kuweka mikakati ya kuongeza fursa za ajira na kuwawezesha kushiriki katika maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Bi. Jenifer Omolo, amesema Serikali inalenga kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii na kuwashirikisha katika kulinda amani.

Naye Mkurugenzi wa The African Initiative for Impact, Bw. Joseph Malekela, amesema Youth for Peace Agenda imetambuliwa na UNESCO kwa mchango wa vijana katika kudumisha amani.

Wakizungumza kwa niaba ya vijana, Mwanaidi Seif na Castal Godwin wamewataka vijana kuendelea kuwa mabalozi wa amani na kushiriki kikamilifu katika kujenga Taifa lenye utulivu na maendeleo.