News
Serikali yaendelea kuimarisha Mafunzo ya Uanagenzi
Serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuimarisha maendeleo ya ujuzi kwa vijana kupitia Programu ya Taifa ya ukuzaji Ujuzi, ambapo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Dkt. Evaline Wilbard Munisi, amefanya ziara katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Sengerema (FDC) kukagua maendeleo ya mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi.
Akizungumza katika ziara hiyo leo Juni 29, 2026, alisema Serikali inalenga kujenga nguvukazi yenye ujuzi, maarifa na ubunifu ili kukidhi mahitaji ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuongeza ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Dkt. Munisi alisema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano inaendelea kutekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa kushirikiana na sekta binafsi kupitia mfumo wa ubia (PPP), huku mafunzo ya uanagenzi yakichukua nafasi muhimu katika kuziba pengo la ujuzi kwa vijana.
Pia Alieleza kuwa mfumo huo unamwezesha mwanagenzi kutumia asilimia 40 ya muda kujifunza nadharia darasani na zaidi ya asilimia 60 kupata uzoefu wa vitendo sehemu za kazi, huku Serikali ikigharamia ada zote za mafunzo hayo kwa asilimia 100.
Aidha, Naibu Waziri alisema katika awamu ya nane ya programu hiyo, Serikali imeboresha mazingira ya mafunzo kwa kuwapatia wanagenzi 5,746 bima ya afya pamoja na posho ya usafiri ya shilingi 100,000 kwa mwezi kwa kipindi cha miezi miwili watakapokuwa kwenye mafunzo ya vitendo. Aliwataka viongozi wa vyuo kuendelea kuwajengea vijana kimaadili, nidhamu, uzalendo na uwajibikaji pamoja na kuimarisha ushauri nasaha na ushirikiano na waajiri ili kuhakikisha wanagenzi wanapata mafunzo yenye tija.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bi. Alana Nchimbi, alisema Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ilianza mwaka 2016/17 ikiwa na lengo la kuongeza ujuzi wa nguvukazi na kukuza ajira nchini. Alibainisha kuwa hadi sasa jumla ya Watanzania 168,657 wamenufaika na programu hiyo kupitia maeneo manne ya utekelezaji ambayo ni mafunzo ya uanagenzi, uzoefu wa kazi kwa wahitimu, urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi.
Bi. Nchimbi alisema katika mwaka wa fedha 2025/26, mafunzo ya uanagenzi yanatekelezwa katika vyuo na taasisi 46 zilizopo katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, yakihusisha vijana 5,746 katika fani mbalimbali. Mkoa wa Mwanza unashiriki kupitia vyuo vitatu ambavyo ni Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Sengerema, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Malya na Pine College, vyenye jumla ya wanagenzi 339.
Mmoja wa Wanagenzi alimshkuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano kwa kuwezesha mafunzo hayo kwa kugharamia ada kwa asilimia 100 na kuwapatia bima ya afya. Walisema tangu kuanza kwa mafunzo Januari 2026 wamepata ujuzi wa kitaaluma, uwezo wa kujitegemea, kujenga mahusiano ya kikazi na mbinu za kupata wateja, huku baadhi yao tayari wakianza kujipatia kipato kupitia ujuzi walioupata.
Hata hivyo, wanagenzi hao waliiomba Serikali kuendelea kushirikiana na waajiri ili kuongeza nafasi za mafunzo kwa vitendo, wakieleza kuwa baadhi ya taasisi na waajiri bado wanatoza fedha ili kutoa nafasi za mafunzo. Walisisitiza kuwa mafunzo ya uanagenzi yamewapa msingi imara wa kujiajiri na kuajiriwa, na kuahidi kutumia ujuzi walioupata kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia uzalishaji, ubunifu na utoaji wa huduma bora.
Mwisho.
