News
Serikali Yahimiza Ubunifu na Matumizi ya Teknolojia kwa Vijana
Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuwezesha vijana kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya ubunifu, uvumbuzi, sayansi na teknolojia kwa lengo la kuchochea maendeleo maendeleo nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi katika Kongamano la Future Ready Summit 2025 lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Aidha, Mhe. Katambi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya maboresho ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana (2007) kwa kutoa toleo jipya la Mwaka 2024 ambayo imehakikisha vijana wanahusishwa katika masuala ya uvumbuzi na ubunifu ili kuibua na kuendeleza vipaji vyao.
Vile vile, amesema shilingi Bil. 1 imetolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa ajili ya kusaidia programu na miradi mbalimbali ya vijana inayolenga masuala ya ubunifu, uvumbuzi na matumizi ya teknolojia.
Aidha, Mhe. Katambi amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kama mratibu wa Wizara za kisekta na msimamizi wa jukumu la Serikali ina hakikisha Sera ya Vijana inatengeneza mazingira mazuri kwa vijana na kuhakikisha wanaendelea kubaki kwenye uchumi na mabadiliko ya teknolojia.
Kadhalika, Mhe. Katambi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuratibu utekelezaji wa sera na programu zinazoshughulika masuala ya maendeleo ya vijana kwa ajili ya Ustawi wa vijana.
Kongamano hilo limeongozwa na kauli mbiu isemayo "Ubunifu Kwa Maendeleo Jumuishiu na yenye Ustahimilivu" na mada isemayo Utafanya Nini ili kujenga uchumi jumuishi Wenye ubunifu Kwa maisha yajayo.