News
Serikali Yaimarisha Miradi ya Kimkakati Kukuza Ajira kwa Vijana
Serikali imeendelea kuwezesha upatikanaji wa ajira kwa vijana kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu inayochochea ukuaji wa uchumi, sambamba na kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 ili kupanua fursa za ajira nchini.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 17, 2026 Bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo alipokuwa akijibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, aliyehoji ni lini Serikali itakuja na mpango madhubuti wa kuhakikisha vijana wanapata ajira za kutosha.
Aidha, Mhe. Kisuo alibainisha kuwa Serikali inaendelea kubuni na kutekeleza programu maalum zinazowawezesha vijana kujifunza kwa vitendo katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira, pamoja na kufanya maboresho ya sera mbalimbali ikiwemo Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023).
Vilevile, Serikali imeanzisha Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi yenye lengo la kuiwezesha nguvu kazi kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira. Hadi sasa, jumla ya Watanzania 168,657 wamenufaika na programu hiyo.
