News
Serikali yapanua fursa za Ajira kwa Vijana kupitia Sekta ya Madini
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo amesema Serikali imeendelea kutekeleza mikakati madhubuti ya kuwezesha vijana kupitia Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Madini ikiwemo ‘Mining for Better Tomorrow’ (MBT) ambapo vijana zaidi ya 5,983 wamewezeshwa mafunzo, mitaji na leseni, vile vile wachimbaji wadogo 658 wakinufaika na mafunzo ya ujuzi.
Amesema hayo leo Aprili 27, 2026 Bungeni, Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mheshimiwa Eng. Chacha Mwita Wambura, Mbunge wa Geita Mjini, ambaye amehoji Je, upi mkakati wa kuunda ajira na kukuza uchumi wa vijana kupitia miradi ya uzalishaji na ujasiriamali ili kupunguza utegemezi wa sekta ya madini.
Akijibu swali hilo, Mhe. Kisuo amesema kuwa Serikali inaendelea kuunda ajira na kukuza uchumi wa vijana kupitia miradi ya uzalishaji na ujasiriamali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza utegemezi mkubwa wa sekta ya madini.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za kuwawezesha vijana kiuchumi ikiwemo programu ya BBT na BBT-LIFE, pamoja na kutoa mikopo yenye masharti nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na pamoja na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.
Mhe. Kisuo amesema hatua hizo zina lengo la kuongeza fursa za ajira, kukuza ujuzi wa vijana ili kuimarisha uchumi wa Taifa.
