Habari

​SIKU YA WATOTO WENYE KICHWA KIKUBWA NA MGONGO WAZI YAADHIMISHWA JIJINI DODOMA

​SIKU YA WATOTO WENYE KICHWA KIKUBWA NA MGONGO WAZI YAADHIMISHWA JIJINI DODOMA

Maadhimisho ya siku ya Watoto wenye kichwa kikubwa (Hydrocephalus) na mgongo wazi (Spina bifida) yamefanyika Jijini Dodoma Oktoba 25, 2018.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jaffo amesema kuwa Serikali imeendelea kuwawezesha watu wenye ulemavu wakiwemo Watoto wenye kichwa kikubwa na mgogongo wazi katika kuhakikisha wanapata huduma mbalimbali ikiwemo huduma za afya, elimu, mafunzo na kuwapatia vifaa saidizi.

“Serikali itaendelea kujenga uelewa kwa jamii kuhusu masuala ya haki za watu wenye ulemavu pamoja na utoaji wa huduma endelevu kwa wenye ulemavu hapa nchini,” alisema Waziri Jaffo.

Aidha, Waziri Jaffo alitoa maagizo kwa kila Halmashauri kutenga bajeti ya shilingi milioni 6 kwa mwaka wa fedha 2019/20 zitakazo kuwa zinawasaidia Watoto hao na asilimia 2% kwa ajili ya kuwawezesha wazazi wenye Watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi.

Aliongeza kuwa, Wakuu wa Mikoa wahakikishe wanasimamia kamati za watu wenye ulemavu vyema kwa kufuatilia kila jambo.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wa Watoto wenye Kichwa Kikubwa na Mgongo Wazi Tanzania (ASBAHT), Bw. Abdulhakim Bayakub alisema kuwa maadhimisho haya yanasaidia kuondoa dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa watu wengi kuhusu tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi.

Naye, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Watu wenye Ulemavu, Bi. Magreth Malunda aliyekuwa amemwakilisha Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa, alieleza kuwa Serikali imedhamiria kuendeleza utekelezaji wa sharia ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya Mwaka 2010 kwa maslahi ya Watu wenye Ulemavu kwa kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya watu wenye ulemavu ili kubadili mitazamo na fikra.

AWALI

Tarehe 25 ya mwezi wa kumi kila mwaka ni siku yam toto wa kichwa kikubwa na mgongo wazi duniani.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Kichwa kikubwa mgongo wazi – Maisha yangu”.