News
TANZANIA YAIMARISHA KINGA YA JAMII KUCHOCHEA UKUAJI WA MIUNDOMBINU- DKT. MUNISI
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, amesema Tanzania imeendelea kuimarisha mazingira ya kisera na kisheria yanayolenga kupanua wigo wa kinga ya jamii kwa ustawi wa wananchi na maendeleo ya uchumi wa taifa.
Dkt. Munisi amesema hayo Oktoba 29, 2026, alipokuwa akizungumza katika Mkutano wa Kwanza wa Bara la Afrika kuhusu Miundombinu ya Hifadhi ya Jamii, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Umoja wa Mataifa jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Mkutano huo una kauli mbiu isemayo "Kuoanisha mifumo ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu na mabadiliko ya kiuchumi barani Afrika."
Akieleza hatua zilizofikiwa na Tanzania, Dkt. Munisi amesema Serikali imeanzisha na kutekeleza Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya 2023, Sera ya Taifa ya Wazee ya 2023, pamoja na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya 2023, ambazo zimeimarisha upatikanaji wa huduma za ulinzi wa jamii kwa wananchi wengi kwa njia jumuishi na endelevu.
"Ni muhimu kuendelea kujenga mifumo ya hifadhi ya jamii iliyo imara kifedha, inayopanua wigo wa kinga ya jamii na kuchangia maendeleo ya kiuchumi yanayowanufaisha wananchi wengi zaidi barani Afrika," amesema Dkt. Munisi.
Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa takwimu za mwaka 2025 zinaonesha mifuko ya hifadhi ya jamii nchini ilikuwa na mali zenye thamani ya takribani Sh trilioni 24.15, sawa na Dola bilioni 9.4, huku asilimia 87 ya mali hizo ikiwa imewekezwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mkutano huo umejadili namna mifuko ya pensheni na taasisi za hifadhi ya jamii barani Afrika zinavyoweza kuoanisha mifumo ya hifadhi ya jamii na uwekezaji ili kuunga mkono agenda ya uendelezaji miundombinu.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Munisi ameongoza ujumbe wa Tanzania unaojumuisha wawakilishi kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Benki ya CRDB.
