News
Vijana 5746 wa Uanagenzi wanufaika na Bima za Afya
✅ Serikali Yaweka Kipaumbele Afya ya Vijana Wanaopata Mafunzo ya Uanagenzi
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imeendelea kuonesha kwa vitendo dhamira yake ya kuwajengea vijana mazingira bora ya kujifunza kwa kuwapatia Bima za Afya vijana 5,746 wanaoshiriki katika Mafunzo ya Uanagenzi Awamu ya Nane (8) ikiwa ni sehemu ya kulinda usalama na afya wa vijana hao katika chote cha mafunzo yao.
Aidha Utoaji wa Bima za Afya kwa wanagenzi hao unaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha maendeleo ya vijana yanaenda sambamba na ustawi wa afya zao, Serikali inaamini kuwa afya bora ni msingi wa mafanikio katika elimu, mafunzo, ajira na uzalishaji, hivyo imeendelea kuweka mazingira yanayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo bila hofu ya gharama za matibabu.
Hatua hiyo pia inaendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa uhakika kupitia mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote.
Kwa mujibu wa Serikali, upatikanaji wa huduma za afya ni haki ya msingi kwa kila mwananchi na nguzo muhimu katika kujenga Taifa lenye watu wenye afya bora, nguvu kazi yenye tija na uwezo wa kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Wanagenzi wanaonufaika na mpango huo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakibainisha kuwa itawapa utulivu wa kupata matibabu wanapohitaji na kuongeza ari ya kujifunza bila kukatishwa tamaa na changamoto za kiafya.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa mafunzo hayo, mwanagenzi wa fani ya Kilimo kutoka Chuo cha Laera Agriculture Centre, Shadrack Mbala, ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano kwa kuwapatia Bima za Afya.
“Huduma hii ni faraja kubwa kwetu. Inaonesha namna Serikali inavyotujali na kuthamini mchango wa vijana katika maendeleo ya Taifa. Sasa tuna uhakika wa kupata matibabu na kuendelea na mafunzo yetu kwa utulivu zaidi,” amesema Mbala.
Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi kupitia Mafunzo ya Uanagenzi imeendelea kuwa moja ya mikakati muhimu ya Serikali katika kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi, maarifa na ushindani katika soko la ajira. Kupitia utoaji wa mafunzo pamoja na huduma za kijamii kama Bima za Afya, Serikali inaendelea kujenga kizazi cha vijana wenye afya bora, ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo endelevu ya Tanzania.
Mafunzo ya Uanagenzi inayotekelezwa katika vyuo 46 nchini imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuwawezesha vijana kupata stadi za kazi zinazohitajika katika sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma. Kupitia mafunzo hayo, vijana hupata uzoefu wa vitendo unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu.
.jpeg)


