Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Vijana Shinyanga Watakiwa kuwa Mabalozi wa Ujuzi Tepe kwa Makundi Maalum


Vijana mkoani Shinyanga walioshiriki katika mafunzo ya ujuzi tepe yanayojikita katika kuwawezesha kujitambua na kujithamini hususani katika ujasiriamali, usimamizi wa biashara na Afya ya uzazi wametakiwa kuwa mabalozi kwa kuendelea kutoa elimu hiyo kwa makundi maalum ambayo ni wenye ulemavu, wamama wadogo (Young Mothers) na wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU).

Akiongea wakati wa Mafunzo hayo yanatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, mjini Shinyanga, tarehe 29 Juni, 2022, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Beda Chamatata amesema suala la vijana kutokuwa na elimu ya ujuzi tepe, limekuwa likisababisha vijana kukabiliwa na changamoto za kiuchumi, kiafya pamoja na kupata mimba katika umri mdogo suala ambalo hupekelea kupoteza dira ya maisha yao.

“Mafunzo haya ya ujuzi tepe yatakuwa msaada mkubwa kwa vijana katika kujitambua, na kufanya maamuzi sahihi juu ya masuala ya maisha yao hii itawawezesha kuzifikia ndoto zao”

Aidha ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuanzisha Programu ya kutoa Mafunzo ya Ujuzi tepe kwa makundi maalumu ya vijana ambayo ni muhimu kwa mustakabali wa maisha ya vijana ambao ni msingi wa maendeleo wa Taifa letu.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Rajabu Masanche, amewaasa vijana hao watakapomaliza mafunzo yao na kuunda vikundi vya ujasiriamali, waendelele kuwa mabalozi kwa kutumia weledi waliopata na kuweza kuzitumia fursa za kupata mikopo ili wapate mitaji na kuanzisha biashara zao kwa kupitia mikopo ya Halmashauri ya 10%, ambapo 4% hutolewa kwa wanawake, 4% kwa vijana, na 2% hutolewa kwa watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Julius Tweneshe, amesema Ofisi hiyo itaendelea kuwawezesha vijana kiuchumi hususani kupita Mfuko wa Maendeleo ya Vijana amabo unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutoa mikopo kwa vijana kupitia Halmashauri.

Wakiongea kwa nyakati Tofauti washiriki wa Mafunzo hayo wameishukuru serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapatia mafunzo hayo ambapo wamesema wataendelea kutoa elimu kwa vijana wengine ili na wao waweze kupata elimu ya kujitambua, pamoja na kufanya maamuzi sahihi kwa manufaa wa maisha yao, na kufanya shughuli za kuwaingizia kipato.