Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Vijana wanavyojenga kesho bora kupitia Mafunzo ya Uanagenzi


Vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa na msingi mkubwa wa maendeleo ya jamii yoyote duniani. Katika kipindi hiki ambacho changamoto za ajira zimeendelea kuongezeka, vijana wengi wamejikuta wakipoteza matumaini baada ya kushindwa kuendelea na masomo au kukosa nafasi za ajira rasmi. Hali hiyo imewafanya baadhi yao kuamini kuwa kufeli masomo ni sawa na kufeli maisha, jambo ambalo limekuwa likisababisha wengi kukata tamaa na kuishi bila mwelekeo sahihi wa maisha.

Kutokana na hali hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano imeendelea kuanzisha programu mbalimbali za kuwawezesha vijana kiuchumi, ikiwemo Programu ya Mafunzo ya Uanagenzi. Programu hiyo imekuwa mkombozi kwa vijana wengi waliokuwa hawana matumaini ya maisha baada ya kushindwa kuendelea na elimu ya juu au kukosa ujuzi wa kujiajiri.

Kupitia mafunzo hayo, vijana wamepata nafasi ya kujifunza ujuzi mbalimbali wa kazi unaowawezesha kujitegemea na kuondokana na utegemezi wa maisha. Mafunzo hayo pia yamekuwa chachu ya kuwafanya vijana kutumia vipaji na nguvu zao katika shughuli za maendeleo badala ya kukaa bila kazi majumbani.

Katika Chuo cha Don Bosco VCT Oysterbay Jijini Dar es Salaam, programu hiyo imeendelea kuleta matumaini mapya kwa vijana wengi wanaopatiwa mafunzo ya uanagenzi katika fani mbalimbali za ufundi na ujasiriamali. Vijana hao wamekuwa wakijifunza kwa vitendo ili kuwajengea uwezo wa kuingia moja kwa moja katika soko la ajira baada ya kuhitimu mafunzo yao.

Vestina Tibakyenda ambaye ni mnufaika wa Mafunzo ya Uanagenzi katika fani ya Uchongaji Vipuli (Fitter Mechanics), amesema kabla ya kujiunga na mafunzo hayo alikuwa nyumbani bila kuwa na shughuli yoyote ya kumuingizia kipato. Amesema kupitia programu hiyo ameweza kupata maarifa na ujuzi mbalimbali ikiwemo masuala ya ujasiriamali pamoja na stadi za maisha (life skills) zitakazomsaidia katika maisha yake ya baadaye.

Vestina ameongeza kuwa mafunzo hayo yameongeza kujiamini kwake na kumfanya kuona kuwa wanawake wana uwezo sawa na wanaume katika fani za ufundi. Hivyo, amewashauri wanawake wenzake kuacha hofu na kujitokeza kujiunga na kozi hiyo kwani taaluma hiyo haibagui jinsia.

Aidha, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwatoa vijana mitaani na kuwapatia mafunzo yenye manufaa ambayo yanawajengea uwezo wa kujitegemea na kuchangia maendeleo ya nchi.

Sambamba na hayo, David Mafua anayesomea fani ya Uchongaji wa Vipuli amesema kabla ya kujiunga na mafunzo hayo hakuwa na ujuzi wala mwelekeo wa maisha, lakini kwa sasa amepata maarifa na stadi zitakazomwezesha kujiajiri mara baada ya kuhitimu mafunzo yake. Kwa kupitia page ya Ofisi ya Waziri Mkuu aliweza kuchangamkia fursa hiyo na kufanikiwa kujiunga, jambo ambalo limekuwa mwanzo mpya wa matumaini katika maisha yake.

Naye, Kelvin Mahundi, anayesomea fani ya Umeme wa Jua (Solar), amesema amechagua fani hiyo kutokana na kuwa na hamasa na uelewa wa awali kuhusu masuala ya umeme, huku akitamani kuwa mtaalamu wa nishati mbadala atakayesaidia familia yake na jamii kwa ujumla.

Amesema kupitia mafunzo hayo ameendelea kupata maarifa ya kina kuhusu uzalishaji na matumizi ya umeme wa jua, jambo ambalo litamwezesha kujiajiri baada ya kuhitimu. Kelvin ameongeza kuwa hadi sasa ana uwezo wa kufanya koneksheni mbalimbali za umeme, kufunga paneli za sola pamoja na kutengeneza switch.

Aidha, Mariam Hamza anayesomea fani ya Umeme wa Jua (Solar) amesema kuwa awali hakuwa na uelewa wowote kuhusu masuala ya solar. Hata hivyo, tangu alipojiunga na chuo hicho na kupata mafunzo mbalimbali, ameweza kujifunza jinsi ya kufunga mfumo wa umeme wa Jua, kuwasha taa pamoja na mambo mengine yanayohusiana na umeme.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwake, na amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha vijana kupata fursa ya mafunzo hayo muhimu.

Kwa upande mwingine, Godfrey Kapinga anayesomea fani ya Uchomeleaji na Uungaji wa Vyuma amesema tangu akiwa mdogo alikuwa na ndoto ya kuwa fundi mahiri wa uchomeleaji wa vyuma, lakini hakuwahi kujua ni kwa namna gani angeweza kufikia malengo hayo kutokana na kukosa fursa na mafunzo sahihi.

Amesema kupitia mafunzo ya uanagenzi anayopata sasa, ameweza kujifunza kwa vitendo namna ya kuchunguza, kutengeneza na kuunda vyuma katika maumbo mbalimbali kulingana na mahitaji. Ameishukuru Serikali kwa kutoa fursa hiyo ambayo imemsaidia kupata ujuzi na kuanza kuona mwanga wa maisha kupitia taaluma hiyo ya ufundi

Naye, Muba Simba amesema tangu zamani alikuwa na ndoto ya kuwa fundi mahiri wa Uchomeleaji na Uungaji wa Vyuma, lakini hakuwahi kupata fursa ya mafunzo ambayo yangeweza kumsaidia kufikia ndoto hiyo.

Amesema kupitia mafunzo ya uanagenzi anayopata sasa, ameweza kujifunza kwa vitendo namna ya kutengeneza mageti, madirisha, fensi pamoja na kazi mbalimbali zinazohusiana na welding, jambo ambalo limemjengea uwezo na kujiamini zaidi katika taaluma hiyo.

Ameishukuru Serikali kwa kumpatia fursa ya kushiriki mafunzo hayo, akieleza kuwa yamekuwa chachu ya maendeleo katika maisha yake na yamemfungulia njia ya kujiajiri na kujitegemea kiuchumi baada ya kuhitimu.

Kwa Upande wa Mkuu wa Chuo cha Don Bosco VTC Oysterbay, Father Felix Wagi, amesema kuwa programu ya mafunzo ya uanagenzi imeendelea kuleta matokeo chanya kwa vijana wengi tangu ilipoanza kutekelezwa chuoni hapo miaka miwili iliyopita. Amesema kwa kipindi hicho wameweza kushuhudia mabadiliko makubwa kwa wanafunzi wanaopata mafunzo hayo, kuanzia tabia, nidhamu, uwezo wa kujitambua hadi namna wanavyojiona katika maisha yao ya baadaye.

Father Wagi amesema vijana wengi walijiunga na programu hiyo wakiwa hawana matumaini, mwelekeo wa maisha wala shughuli za kuwaingizia kipato, lakini kupitia mafunzo hayo wameanza kupata mwanga mpya wa maisha na kujiamini zaidi.

Ameeleza kuwa programu hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa vijana kwani inawajengea stadi za kazi, maarifa ya ujasiriamali pamoja na uzoefu wa vitendo unaowasaidia kujitegemea. Amesema tofauti kubwa inaonekana kwa wanafunzi tangu walipojiunga hadi sasa, ambapo wengi wao wameweza kutambua uwezo wao, malengo yao ya maisha na namna ya kutumia ujuzi wanaoupata kujiletea maendeleo binafsi na kusaidia jamii inayowazunguka.

Father Wagi ameongeza kuwa vijana wengi waliokuwa wamekata tamaa kutokana na changamoto mbalimbali za maisha sasa wameanza kuona thamani yao katika jamii na kutambua kuwa wana nafasi kubwa ya kufanikiwa kupitia elimu ya ufundi na stadi za kazi. Amesema mafunzo hayo yamewasaidia vijana kuelewa uhalisia wa maisha, kuwajengea nidhamu ya kazi na kuwapa uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao ya baadaye.

Aidha, ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano kwa kuendelea kuwekeza katika programu za kuwawezesha vijana, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira na kuwajengea vijana Taifa lenye nguvu kazi yenye ujuzi na tija.

Kwa ujumla, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano imeendelea kuonyesha dhamira ya kweli ya kuwainua vijana kwa kuwapatia mafunzo na fursa mbalimbali za ajira ndani na nje ya nchi. Kupitia programu za mafunzo ya uanagenzi, vijana wengi wanaendelea kupata matumaini mapya ya maisha, kujitegemea kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.