Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Vijana Wapongeza Serikali Mafunzo ya Uanagenzi, Wasema Yafungua Milango ya Ajira na Kujitegemea


Vijana wameipongeza Serikali kwa kuwekeza katika maendeleo yao na kuwapa fursa ya kukuza ujuzi kupitia Mafunzo ya Awamu ya Nane ya Stadi za Kazi kwa Njia ya Uanagenzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Mafunzo hayo yanaratibiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, ambapo vijana wanagharimiwa mafunzo kwa asilimia 100 hatua inayowaondolea vikwazo vya kifedha na kuwapa nafasi sawa ya kushiriki na kunufaika na programu hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, vijana hao, wamesema fursa hiyo imewajengea msingi imara wa kujiamini, kuwapa uzoefu wa moja kwa moja katika mazingira halisi ya kazi na kuwafungua milango ya ajira rasmi pamoja na kujiajiri.

Wameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo, wamepata maarifa ya vitendo yanayohitajika katika soko la Ajira, hivyo kuongeza ushindani wao katika soko la ajira na kuwapa matumaini mapya ya kujitegemea kiuchumi.

Kwa upande wake, Baraka Dickson, mnufaika wa Mafunzo ya Uanagenzi kutoka Chuo cha Mitambo (IHET), amesema kupitia mafunzo hayo amepata ujuzi wa vitendo uliomwezesha kujiajiri na sasa anapata kipato cha uhakika kinachomsaidia kuhudumia familia yake na kuboresha maisha yake kwa ujumla.

Naye, Helen Odielo, mnufaika wa Mafunzo ya Uanagenzi mwenye mahitaji maalum kutoka Chuo cha Ufundi Don Bosco, ameiomba Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki na jumuishi kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo kuhakikisha wanapewa kipaumbele stahiki katika utekelezaji wa asilimia 3 ya ajira zinazotengwa kwa ajili yao ili wanufaike kikamilifu na fursa za Ajira.

Aidha, mnufaika wa Mafunzo ya Uanagenzi kutoka Chuo cha Mitambo IHET, Thomas Marwa, amesema mafunzo hayo yamempa ujuzi stahiki wa vitendo, kumwezesha kuajiriwa baada ya kumaliza mafunzo hiyo.

Akifungua mafunzo hayo Machi 3, 2026 kwa Vijana 5,746 waliodahiliwa katika Vyuo 46 nchini kwa mwaka 2025/26, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amesema Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa changamoto yoyote itakayojitokeza kwa vijana wawapo kwenye mafunzo na baada ya mafunzo.

Waziri Sangu ameongeza kuwa Serikali itahakikisha kila fani inayotolewa ina idadi ya wanafunzi wanao maliza programu ya mafunzo ya uanagenzi wanaunganishwa na fursa za miradi kupitia zabuni za Serikali ili kuhakikisha ujuzi waliopata unatumika kikamilifu.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Stadi, Mkuu wa Chuo cha Ufundi kupitia programu ya uanagenzi, Mkuu wa Chuo cha Don Bosco Eng. Dkt. Justine Mulebya, amesema mafunzo hayo yamewezesha Vijana wengi nchini kupata ujuzi stahiki kazi, kuwapa nafasi ya kuajiriwa au kujiajiri.