Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Vyama vya Wafanyakazi si Wachochezi - Naibu Waziri Katambi


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi, amesema kuwa vyama vya wafanyakazi vina nafasi kubwa katika kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira rafiki kwa kupambana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza kati ya watumishi na serikali na si chanzo cha uchochezi kwa wafanyakazi kama inavyoonekana na baadhi ya watu.

Naibu Waziri Katambi aliyasema hayo alipokuwa akifunga mkutano mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Technolojia, Ufundi Stadi, Habari na Utafiti (RAAWU) tarehe 08 aprili, 2022 katika ukumbi wa Royal Hotel jijini Dodoma.

‘Mwenyekiti wenu kaeleza hapa hata katika hotuba nimesikia ikiongelewa kuwa vyama vya wafanyakazi ni wachochezi wa wafanyakazi, mimi leo hii kwa niaba ya serikali naomba nitamke nyinyi sio wachochezi, mtu anayekwambia ukweli ni mtu muhimu sana kumsikiliza badala ya kumuangamiza. Nyie mnatusaidia sana kupunguza manung’uniko ya wafanyakazi katika maeneo yenu” alisema Mhe. Katambi.

Akiongelea kuhusu wafanyakazi wanaokaimu nafasi kwa muda mrefu bila kuthibitishwa, alisema baadhi ya Taasisi zinachukua muda mrefu kujaza nafasi za uongozi zinapotokea hali inayosabisha kutengeneza ombwe la uongozi linaloathiri utekelezaji wa majukumu ya Taasisi na kushusha morali na hali ya kufanya kazi kwa watumishi wanaoachwa kukaimu nafasi za uongozi kwa muda mrefu.

‘Utaratibu wa kukaimu nafasi za uongozi unakusudiwa kuwa ni wa mpito wakati taratibu za kujaza nafasi hizo rasmi ukiendelea, waajiri watakao bainika kutozingatia sheria na miongozo ikiwemo ile inayohusisha stahili za watumishi watachukuliwa hatua’ alisema Mhe. Katambi.

Amefafanua kuwa serikali imeweka utaratibu wa kufuata ili kujaza nafasi za uongozi katika utumishi wa umma na taratibu hizo zina lengo la kuhakikisha watumishi wanaoteuliwa kujaza nafasi za uongozi na wenye sifa stahiki.

Vilevile alisema kuwa Taasisi za Serikali hazina hiari katika kuzingatia matakwa ya kisheria ya kulipa stahiki mbalimbali za watumishi ikiwemo stahiki za gharama za likizo hivyo serikali itafanya kaguzi na kuhimiza kufuata kanuni sheria na utaratibu zilizopo katika usimamizi wa rasilimaliwatu.

Aidha ameeleza kuwa changamoto ambazo zinahusu wafanyakazi Wizara itaendelea kushirikiana na chama cha RAAWU ili kuweza kuangalia namna ya kuweza kuzitatua na changamoto ambazo zinahusu taasisi viongozi kwa kushirikiana na watumishi kupitia vikao vitajadili chngamoto hizo ili kuweza kuzitatua.