Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAAJIRI SEKTA BINAFSI SASA KULIPA ASILIMIA 0.6 YA MICHANGO YA WAFANYAKAZI KWENYE MFUKO WA WCF


WAAJIRI kutoka Sekta Binafsi sasa watalipa asilimia 0.6 ya michango ya wafanyakazi wao kwenda Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) badala ya asilimia 1 ya awali kuanzia Tarehe 1/7/2021, WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mheshimiwa Jenista Mhagama (MB), amesema leo Juni 13, 2021 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakati walipotembelea ofisi za WCF jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo mbalimbali ya Kamati ikiwemo kuwekeza katika mifumo ya TEHAMA na uboreshe mfumo wa tathmini ya madai, alisema waajiri kutoka Sekta ya Umma wataendelea kulipa kiwango cha awali cha asilimia 0.5.


“Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani alitoa maelekezo kwa kila
taasisi ya serikali iweke mazingiza mazuri ya kuvutia wawekezaji na kupunguza kero zilizokuwa zinaleta changamoto, bila ya kupoteza muda Ofisi ya Waziri Mkuu imeanza kuchukua hatua, na katika kero kubwa iliyokuwa inawakwaza wawekezaji na waajiri nchini hasa Sekta Binafsi ni ule uwiano wa michango asilimia 0.5 Sekta ya Umma na asilimia 1 kwa sekta binafsi, sasa tumetekeleza kwa kuondoa huo
mzigo wa uchangiaji.”
Alisema Mheshimiwa Waziri.

Pia Mheshimiwa Waziri alisema sambamba na hilo, Serikali kupitia WCF inafikiria kufuta malimbikizo ya madeni ya michango ya huko nyuma ili kuwepo kwa mazingira mazuri kwa waleWaajiri ambao hawajajisajili ili waweze kujisajili na isiwe kikwazo kwao na waliojisajili watekeleze wajibu wa kulipa michango.



Alisema kipaumbele cha Serikali ni kuimarisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ili uendelee kulipa fidia kwani huduma za hifadhi ya jamii ni haki ya kikatiba.

“Hifadhi ya jamii ni haki ya kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 11 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. Ibara hii inaipa Serikali wajibu wa kuweka mazingira ya kisera na kisheria kwa lengo la kuhakikisha, pamoja na mambo mengine, kwamba kila mwananchi anapata kinga wakati wa uzee, ugonjwa au ulemavu.” Alifafanua Mheshimiwa Mhagama.

Waziri huyo aliwahakikishia wajumbe hao kuwa ripoti ya mtathmini (Acturial report) imeonyesha kazi ya Mfukoni nzuri na Mfuko unaendelea vema na kuitaka Menejimenti iendelee kuchapa kazi kwa kujituma na kuweka uzalendo mbele.



“Katika uhai wake wa miaka sita tangu uanzishwe Mfuko umekutekeleza takwa hilo la kikatiba kwa mafanikio makubwa ambapo mwaka 2015-2016 ulilipa Fidida ya Shilingi Bilioni 1.55 na sasa Fidia imefikia hadi shilingi bilioni 9.05.

Kwa upande wake Makamu Mwenyemkiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Najma Giga alisema, Kamati yake imeridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Mfuko katika kutekeleza maelekezo ya Kamati ambapo hivi sasa huduma za Mfuko zimerahisishwa kufuatia matumizi ya TEHAMA ambapo huduma mbalimbali zinafanyika kidigitali.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma alieleza mafanikio mbalimbali katika upande wa makusanyo ya michango, mifumo ya kutolea huduma, uwekezaji, malipoya fidia na katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yake, Mfuko umekuwa ukipata hati safi ktoka kwa Mkaguzi Mkuu.



“Pamoja na mafanikio haya pia kuna changamoto kama vile uelewa mdogo, lakini pia waajiri kutowasilisha nyaraka za ukweli na sahihi, lakini pia Mfuko unaelekeza nguzu zake katika kuhakikisha unaondoa changamoto ya madaktari kwa kuendelea kutoa mafunzo nchi nzima.” Alisema Dkt. Mduma.