Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Wadau Wahamasishwa Kutekeleza Sera ya Kinga ya Jamii


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ametaka wadau wa sekta ya Kinga ya Jamii kujipanga vyema na kuweka nguvu katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, amesema Sera hiyo imeonesha mwelekeo wa Sekta ya Kinga ya Jamii nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wote wenye uwezo wa kuzalisha kipato wanajiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema hayo wakati akifunga Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Kinga ya Jamii uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC), leo Februari 10, 2026, Jijini Arusha.

Amesema kuwa, ndoto ya Watanzania kuwa ndani ya mfumo wa hifadhi ya jamii sasa inakwenda kukamilika kutokana na uwepo wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii, hivyo amepongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ya kuandaa sera hiyo muhimu kuhusu kinga ya jamii.

Vilevile, Waziri Ridhiwani Kikwete ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya Kinga ya Jamii kuyaishi maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo aliyatoa wakati wa kuhitimisha Bunge la 12, tarehe 27 Juni 2025 kuhusu utekelezaji wa sera hiyo pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo lengo la pili linasisitiza Maisha Bora na Ustawi wa Wote.

Ameongeza kuwa, mpaka sasa maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yameleta mafanikio makubwa katika sekta hiyo ambayo yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 17 zenye utaratibu bora wa kinga ya jamii.

Akizungumza awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mary Maganga akimkaribisha waziri Kikwete alisema Mkutano huo wa siku mbili umetoa fursa kwa wadau kujadili kwa kina na kubadilishana uzoefu katika kuboresha sekta hiyo kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

“Mkutano huu ulilenga kukuza uelewa kwa umma kuhusu umuhimu wa kinga ya jamii sambamba na kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine ili kuimarisha sekta ya kinga ya jamii nchini,” amesema