Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAJUMBE KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA YATEMBELEA KIWANDA CHA SIGARA TANZANIA (TCC) NA KIWANDA CHA KNAUF KINACHOZALISHA GYPSUM BOARD


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wamefanya ziara katika ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ili kujionea jinsi Taasisi hiyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inavyosimamia uzingatiaji wa viwango vya usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.

Ziara hiyo imetokana na taarifa ya utekelezaji majukumu ya OSHA kwa mwaka 2020/2021 iliyowasilishwa kwenye Kamati hiyo mwezi Machi ambapo Kamati iliridhishwa na utendaji na hivyo kuagiza kuandaliwa kwa ziara kwa ajili ya Kamati kuona uhalisia wa masuala ambayo wamekuwa wakiwasilishiwa kupitia taarifa mbali mbali.




Akizungumza baada ya kutembelea ofisi za OSHA, kiwanda cha Sigara (TCC) na kiwanda cha Gypsum cha Knauf (Knauf Gypsum Tanzania Limited) kilichopo Mkuranga ambako walikwenda kutazama jinsi viwanda hivyo vinavyotekeleza miongozo inayotolewa na OSHA, Kaimu Mwenyekiti Kamati hiyo, Najma Murtaza Giga, amesema wameridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na OSHA katika kutoa miongozo ya kulinda nguvu kazi katika maeneo ya kazi hapa nchini.

“Ziara yetu imefana na suala tulilolifuatilia la usalama na afya mahali pa kazi kwakweli hapa tumeona linazingatiwa ipasavyo jambo ambalo linapelekea kampuni hii kufanya vizuri katika uzalishaji. Hivyo tumefurahi sana na tunaamini kwamba mtaendelea kufanya vizuri, amesema Najma Murtaza Giga, Kaimu Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria.


Aidha, baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wakiwa wameambatana na Mwenyekiti wao wamesema kupitia ziara hiyo wameweza kutambua kazi kubwa inayofanywa na OSHA katika kuhakikisha kwamba mazingira ya kazi yanakuwa salama.

“Nitumie fursa hii kuipongeza menejimenti ya OSHA pamoja na Waziri Jenista Mhagama kwa kazi kubwa wanayofanya. Kiukweli wakati mwingine unaweza usione umuhimu wa Taasisi hizi kama usipofika katika maeneo wanayoyasimamia. Sisi leo, tumejionea wenyewe kazi kubwa inayofanywa na OSHA katika kutoa miongozo na ushauri wa namna ya kuboresha mazingira ya kazi. Sisi kama wabunge tuna kazi kubwa ya kuunga mkono kazi hii na kuishauri serikali kuiongezea OSHA bajeti ili iweze kupanua wigo wa shughuli hizi za ukaguzi katika maeneo ya kazi”. Amesema Elibariki Kingu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mjumbe Kamati.


Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amesema serikali imekuwa ikitegemea sana ushauri wa Kamati za Bunge ili kuweza kutekeleza mipango yake ipasavyo.

“Sisi kama serikali tunaweza tukawa tunajifungia ndani na kutengeneza mipango mbali mbali ya maendeleo lakini ili mipango hiyo iweze kutekelezeka na kuwa na tija kwa wananchi tunategemea sana ushauri kutoka kwa wabunge hususan Kamati ya Katiba na Sheria ambao ndio wawakilishi wa wananchi”. Amesema Waziri Mhagama.



Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema kupitia ziara hiyo wajumbe wa Kamati wamepata fursa ya kujionea hali halisi ya usalama na afya katika maeneo ya kazi hapa nchini.

“Kupitia ziara hii waheshimiwa wabunge wamejione jinsi ambavyo OSHA imejipanga kulinda nguvu kazi ya nchi na kwakweli wamefarijika sana na wamekiri kwamba yale ambayo wamekuwa wakiyaona katika taarifa zetu ndiyo ambayo tunayatekeleza katika sehemu za kazi na hivyo kupelekea wawekezaji kupata tija katika uzalishaji”. Alieleza Kiongozi Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda.