News
Wakulima wa Maharage Wanufaika Mafunzo ya Ukuzaji Ujuzi
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imeendelea kutoa mafunzo kwa vitendo ya ukuzaji ujuzi kwa wakulima wa zao la maharage ikiwa ni jitihada za kuwawezesha kuongeza tija na thamani ya mazao wanayozalisha.
Akizungumza leo Januari 14, 2026 Jijini Mbeya, Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Ajira Ofisi hiyo, Godwin Mpelumbe, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ufanisi na tija katika uzalishaji wa zao la maharage, kukuza uwezo wa kiushindani na kuwaongezea wakulima maarifa ya kibiashara ili waweze kuongeza thamani ya zao hilo.
Aidha, Mpelumbe amesema Kupitia mafunzo hayo, wakulima wanawezeshwa kubadili kilimo cha mazoea na kujikita katika kilimo cha kibiashara.
Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Esther Kunyanja ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa mafunzo hayo yenye manufaa makubwa kwa wakulima, na kuiomba Serikali kuendeleza programu hiyo katika mikoa mingine ili kuwawezesha wakulima wengi zaidi kupata ujuzi wa kisasa.
