Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Wamiliki wa Viwanda watakiwa kutoa Mikataba ya Kazi kwa Wafanyakazi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewataka wamiliki wa viwanda nchini kutekeleza ipasavyo sheria za kazi ikiwemo kuwapa mikataba ya kazi wafanyakazi wanaowaajiri ili kuepukana na migogoro mahali pa kazi.

Akiongea baada ya kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa sheria za kazi na Waajiri katika maeneo ya kazi ya viwandani jijini Mwanza, Waziri Ndalichako amefafanua kuwa suala kubwa alilobaini katika ziara hiyo kuwa wapo wafanyakazi ambao hawana mikataba kabisa ya kazi aidha ya kudumu au ya muda mfupi.

“Wafanyakazi wengine wameajiriwa kwa zaidi ya miaka kumi na tano lakini wanakuwa wanapewa mkataba wa mwezi mmoja mmoja, sheria za mikataba ya wafanyakazi zinaweka wazi juu ya aina ya kazi ambazo mfanyakazi anaweza kupewa mkataba wa kudumu au wa muda mfupi"

Amesisitiza kuwa Mikataba mingine huandaliwa tu kwa ajili ya kutuonesha watendaji wa serikali lakini wafanyakazi hawana nakala hizo na hata wakati wa kusaini wafanyakazi hawajui kilichomo ndani ya hiyo mikataba,”

Aidha, amesisitiza kuwa suala la Usalama na Afya mahala pa kazi bado ni changamoto katika viwanda vingi hususan katika kuwapatia vifaa kinga wafanyakazi wakati wa shughuli za uzalishaji viwandani, hivyo ameielekeza OSHA kutoa elimu ili kuhakikisha sheria ya Usalama na Afya mahala pa kazi inatekelezwa.

Mhe. Ndalichako amefafanua kuwa utekelezaji wa sheria za kazi bado kuna mapungufu hususan katika kulipa michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

“Ni wasihi waajiri wahakikishe wanakuwa na takwimu sahihi za michango wanayowasilisha katika mifuko ya hifadhi ya jamii, kwani idadi ya wafanyakazi wanaochangiwa katika mfuko wa NSSF tumekuta inakuwa tofauti sambamba na michango ya mfuko wa WCF, ikiwa idadi ya wafanyakazi walio ajiriwa ipo hivyo, mnapaswa kuhakikisha takwimu hiyo inaoana na waliochangiwa katika mifuko ya Hifadhi ya jamii”

Aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuvutia wawekezaji nchini.