News
Wataalam wa Ustawi Jamii Watakiwa Kuzingatia Maadili
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo amewataka wataalamu na wadau wa Ustawi wa Jamii kufanya kazi kwa weledi, uadilifu katika utendaji kazi hususani kwa watoto na wananchi wanyonge.
Kisuo amewataka wataalam hao kutumia teknolojia (mifumo ya Kielektroniki) katika utendaji kazi ili kurahisisha ukusanyaji wa taarifa mbalimbali.
Naibu Waziri huyo amezungumza hayo (24 Machi 2026 ) wakati wa alipofungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii Tanzania (TASWO) uliofanyika katika Ukumbi wa Lavenda jijini Dodoma.
Kuhusu umuhimu wa kada hiyo nchini, Naibu Waziri alisema kuwa wataalamu wa Ustawi wana nafasi kubwa ya kuimarisha uhusiano katika jamii ili kuleta amani na utulivu kwa jamii.
Sambamba na hayo, Naibu Waziri Kisuo aliongeza kusema kutokana na Ofisi yake iliyo na dhamana ya kuratibu Mahusiano baina ya Serikali na Makundi ya Kijamii yanayojumuisha Siasa, Taasisi za Dini, Asasi za Kiraia na Mashirika yasiyo ya Kiserikali, wao kama Wataaluma wana nafasi kubwa katika kuimarisha Mahusiano haya baina ya Serikali na Makundi ya kijamii katika ngazi mbalimbali za kiutawala.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama wa wataalamu wa Ustawi wa Jamii (TASWO) Dkt. Mariana Makuu akizungumza kwenye kikao hicho alisema kongamano limelenga kuwakutanisha wanataaluma wa huduma za ustawi wa jamii, watunga sera ,wanafunzi na wakufunzi kutoka vyuo vinavyotoa taaluma za ustawi wa jamii ili kujadili kwa pamoja maswala ya kitaalamu kwa lengo kuu la kuboresha elimu ,sera na huduma za utawi wa nchi.
Kwa upande Mwingine Dkt.Mariana ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi ambayo imeifanya katika kuboresha elimu ya ustawi wa jamii, huduma za ustawi wa jamii pamoja na mazingira ya utoaji wa huduma pia na kuendelea kuimarisha mifumo ya maendeleo nchini .
Naye Kamshna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu Bw.Mussa Mkamate alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, taasisi mbali mbali ili kuhakikisha kwamba huduma za ustawi wa jamii zinatolewa kwa viwango vinavyo stahili .
Bw.Mussa aliwahimiza maafisa ustawi wa jamii kuwa waaminifu na waadilifu katika utendaji kazi wao na kuwataka TASWO kuwachagua viongozi waadilfu watakao kuwa kiungo kati ya chama hicho na Serikali.
