Habari

WAWEKEZAJI WASHAURIWA KUFUATA SHERIA ZA KAZI

WAWEKEZAJI WASHAURIWA KUFUATA SHERIA ZA KAZI

Wawekezaji washauriwa kufuata taratibu, kanuni na Sheria za kazi zilizopo nchini ili kuongeza tija na ufanisi katika sekta hiyo ya kazi.


Hayo ameyasema na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea Shamba la Katani la China State Farms lililopo wilayani Kilosa ikiwa ni ziara yake ya kutembelea maeneo ya kazi.


Akizungumza mara baada ya kuwasili katika shamba hilo alieleza kuwa wawekezaji wakiwa kama waajiri lazima wahakikishe wanafuata sheria za kazi katika maeneo yao ya uzalishaji kwa kuzingatia masuala ya msingi ya wafanyakazi ili waweze kuzalisha kwa tija na kuwahamasisha kufanya kazi zao kwa juhudi.


“Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeendelea kuboresha mazingira ya biashara ambayo yamekua yakivutia zaidi wawekezaji, hivyo sera nzuri zilizopo nchini zimekuwa chachu kwa wawekezaji kuwekeza katika nchi yetu,” alisema Mhagama

Alieleza pia, endapo wawekezaji watafuata miongozo ya kisheria katika masuala ya kazi na ajira yatawarahisishia utendaji wao wa kazi.


Akitolea mfano kuhusu masuala ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi, likizo ya uzazi kwa wanawake, uwazi wa mikataba ya ajira, uhuru wa mfanyakazi kujiunga na chama cha wafanyakazi, haki ya kupatiwa vitendea kazi na maslahi ya wafanyakazi ni baadhi ya vitu vya msingi ambavyo mwekezaji inabidi atoe kwa mfanyakazi wake kwa kuzingatia taratibu na sheria.

Hata hivyo aliongezea kuwa ushirikiano na vyama vya wafanyakazi ni jambo la muhimu kwa kuwa vimekuwa vikitetea masuala ya wafanyakazi ambayo yamekuwa yakijitokeza katika maeneo yao ya kazi, pamoja na kuwa na mkataba wa hali bora za wafanyakazi baina ya mwajiri na mwajiriwa.


Sambamba na hilo Mheshimiwa Mhagama alitoa maagizo kwa timu ya wataalamu ambao aliambatana nayo kutoka Idara ya Kazi, Wakala wa Usalama na Afya mahala pa Kazi (OSHA), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya jamii (NSSF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Tume ya Usuluhisi na Uamuzi pamoja na Viongozi wa vyama vya Wafanyakazi kuendelea kutoa elimu kwa umma hususan wafanyakazi ili watambue sheria za kazi na namna taasisi hizo zinaweza kuwasaidia katika kupata ufumbuzi wa masuala yao ya kazi.


Aidha, Waziri Mhagama alitoa pongezi vilevile kwa wawekezaji wa Shamba la Katani la China State Farms kwa kuwajali wafanyakazi wao ikiwa na kuwajengea nyumba bora za kuishi wafanyakazi wao.


“Nimpongeze mwekezaji kwa kuona umuhimu wa kuwajengea makazi wafanyakazi ambayo yatamaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa nyumba na umbali ambao wafanyakazi wamekua wakitumia kwenda kazini,” alisema Mhagama

Pia, alitumi muda huo kuwahamasisha wafanyakazi kutumia muda wao wa ziada katika mashamba yao binafsi na kujiunga kwenye mashamba ya ushirika yatakayo wawezesha kupata soko la uhakika kutoka kwa mwekezaji huyo ili waweze kuimarika kiuchumi.


Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Adam Mgoyi alisema kuwa Sheria za kazi zimekuwa zikitoa mwongozo mzuri kwa wawekezaji katika kuimarisha shughuli zao za uzalishaji, kutoa ajira pamoja na kuchangia kwenye mapato ya nchi.


Kwa upande wake, Meneja wa Kiwanda hicho Bw. Majuto Chitema alitoa pongezi zake kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusifu juhudi alizonazo katika kuboresha na kuwajengea mazingira wezeshi wawekezaji, kwani serikali yake imeweza mstari wa mbele kuweka sera, miongozo, kanuni na sheria ambazo zimekuwa haziwabani wawekezaji.


Miongoni mwa Wafanyakazi wa China Estate Farms Bw. Azory Andrea alisema kuwa Serikali iendelee kuangalia namna ya kuwa kuwasimamia wawekezaji waliopo nchini ili waweze kutekeleza wajibu wao kwa wafanyakazi kwa mujibu wa sheria za kazi.

Kabla ya ziara hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama aliwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kupata taarifa ya maeneo aliyoandaliwa kutembelea katika ziara yake mkoani hapo.