Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MHAGAMA AAGIZA HALMASHAURI KUSHIRIKISHA WATU WENYE ULEMAVU PROGRAMU YA MAFUNZO YA KILIMO CHA KITALU NYUMBA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameagiza halmashauri zitakazojengwa vitalu nyumba kushirikisha vijana wenye ulemavu.

Waziri Mhagama ameyasema hayo alipofanya ziara ya kikazi Mkoani Ruvuma na Iringa kukagua maeneo yatayojengwa na kutoa mafunzo kwa vijana kupitia teknolojia ya kitalu nyumba (Green House).

Akizungumza wakati wa ziara hiyo alisema kuwa katika halmashari zote 83 ambapo teknolojia ya kilimo cha kitalu nyumba itaanzishwa, idadi ya vijana 100 watakaopata mafunzo hayo ijumuishe na wenye ulemavu.

“Halmashauri zitengeneze mfumo madhubuti wa kuwashirikisha vijana wenye ulemavu katika mradi huu, kwani wanaouwezo wa kufanya kazi kama ilivyo vijana wengine na wakiwezeshwa wanaweza”, alisema Mhagama.

Pamoja na hayo, Mhagama amehimiza halmashauri hizo zisimamie vyema mradi huo kwa kuufanya unakuwa endelevu na kuwaunganisha vijana kwenye vyama vya akiba na mikopo ili waweze kupata mikopo itakayowawezesha kujiendeleza kiuchumi kupitia programu hiyo.

Aliongeza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu imeshakamilisha maandalizi yote ikiwemo wataalamu watakao fundisha vijana kujenga kitalu nyumba, kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji, upandaji wa miche na kuwaelimisha mifumo mizuri ya kutafuta masoko.

Naye, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bw. Lucas Kambelenjo amemuhakakikishia Mhe. Waziri kusimamia ipasavyo mradi huo na kuahidi kutekeleza maagizo aliyoyatoa pamoja na kuwahamasisha vijana zaidi kushiriki katika kujifunza teknolojia hiyo mpya ya kilimo cha Kitalu Nyumba.

Waziri Mhagama alifanya ziara hiyo Mbinga Mji eneo la Mji Mwema, Nyasa na Mkoga, Iringa. Mradi huo unategemea kuanza kwenye Mikoa 12 ikiwemo ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Mwanza, Simiyu, Geita, Kagera, Manyara, Lindi, Shinyanga na Kilimanjaro.