Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MHAGAMA ARIDHISHWA NA HATUA YA UJENZI WA MAJENGO YA SERIKALI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe.Waziri Mhagama ametembelea na kukagua ujenzi wa majengo ya Ofisi za Serikali katika eneo la Mji wa Serikali Ihumwa Dodoma na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa.

Mpango wa Utekelezaji wa ujenzi huo kwa awamu ya kwanza umefikia asilimia 82 na unatarajiwa kukamilika Januari 2019 ambapo Viongozi na baadhi ya watumishi wanapaswa kuwa wamehamia katika eneo hilo mapema mwakani.

Waziri Mhagama alitembelea eneo hilo tarehe 8 Desemba, 2018 na ameeleza kufarijika kwa hatua za awamu ya kwanza za maandalizi ya ujenzi zilizofikiwa na kila Wizara.

“Nimeridhishwa na hatua zilizofikiwa kwa wizara zote ambapo hadi sasa Wizara 21 zimepewa maeneo na tayari wameanza kusafisha, na hatua za awali za ujenzi kwa kuzingatia maelekezo ya TBA wakiwa ndiyo wasimamizi wa ujenzi wa majengo”.alieleza Mhagama

Waziri Mhagama aliongezea kuwa, adhma ya Serikali ni kuhakikisha inajenga majengo bora yenye kuzingatia mahitaji yote muhimu ikiwemo miundombinu ya umeme, maji safi na taka, TEHEMA, Mawasiliano na barabara katika mji wa Serikali Ihumwa.

Amesema mbali na hatua hiyo ya kwanza Serikali itaendelea kujenga kwa hatua zingine ambapo baada ya awamu ya kwanza ya majengo ya awali Kila wizara itaendelea na ujenzi wa majengo makubwa kwa kadiri Wizara hizo zitakavyokuwa zikitenga fedha kila mwaka.

Waziri Mhagama alipongeza kazi inayoendelea kufanywa na Vikosi kazi vya ujenzi, Wakala wa Majengo pamoja na waratibu wa zoezi hilo la kuhakikisha Serikali Dodoma kama ilivyopangwa.

“Kipekee niwapongezi watendaji wote wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma kinachoongozwa na Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi ya kuendelea kuratibu zoezi hili”.alisisitiza Mhagama.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Prof.Faustin Kamuzora ameeleza furaha yake ya kuendelea kuenzi mawazo ya hayati baba wa Taifa Mwl.Nyerere kwa vitendo na kuona ni tukio la kihistoria katika nchi ya Tanzania.

“Hili ni tukio la kihistoria linalopaswa kuandikwa katika vitabu na kumbukumbu za nchi yetu ikiwa ni wazo lililoazishwa na baba wa Taifa, na kutekelezwa kuanzia mwaka 2016 Serikali ilipohamia rasmi Dodoma”.Alisisitiza Prof.Kamuzora

Aidha aliongezea kuwa, Watumishi wa Serikali pamoja na jamii yote wanapaswa kuunga mkono jitihada hizi za Serikali kuhamia Dodoma kwa kuendeleza mji na kujiletea maendeleo kwa kuwajibika kwa bidii na kujishughulisha katika shughuli za uzalishaji mali wawapo Dodoma.