Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MHAGAMA ATOA MAAGIZO KWA TAASISI NA HALMASHAURI ZISIZO NA MABARAZA HAI YA WAFANYAKAZI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ametoa maagizo kwa Taasisi na Halmashauri zisizo na mabaraza hai ya wafanyakazi kuunda haraka mabaraza ya wafanyakazi ili mabaraza hayo yaweze kutekeleza sera ya ushirikishwaji mahala pa kazi.

Hayo ameeleza wakati alipokuwa akifungua kikao cha Baraza Mkuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kilichofanyika ukumbi wa Mkutano Royal Hoteli Jijini Dodoma tarehe 14 Januari, 2021.

Waziri Mhagama alieleza kuwa Mabaraza ya Wafanyakazi ni chombo muhimu na ni chachu ya mahusiano mazuri baina ya waajiri na wafanyakazi katika maeneo ya kazi, pia ni moja ya nguzo kuu katika ushirikishwaji wa wafanyakazi ambapo wafanyakazi kupitia uwakilishi wao na viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanapata fursa ya kutoa ushauri na kushiriki namna ya kutekeleza majukumu ya sekta ya kazi.

“Zipo baadhi ya Halmashauri na baadhi ya Taasisi ambazo hazifanyi vikao vya mabaraza ya wafanyakazi ipasavyo na Halmashauri nyingine hazijahuisha Mabaraza ambayo muda wake umeisha,” alisema Mhagama

“Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka 2020 jumla ya Halmashauri 185 kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni Mabaraza 123 tu ndio yapo hai, huku Mabaraza ya 62 hayapo hai, nichukue fursa hii kuziagiza Halmashauri husika kuunda Mabaraza hayo na kukaa vikao vya mabaraza kwa Mujibu wa Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali na kuhuisha mabaraza hayo,” alieleza

Aliongeza kuwa Taasisi zote ambazo hazijaunda mabaraza na ambazo zimeunda kuhuisha mikataba ya mabaraza hayo na kukaa vikao. Pia amezitaka Taasisi kutenga bajeti ya utekelezaji wa shughuli za mabaraza kutokana na umuhimu wa mabaraza haya katika ulimwengu wa kazi.

Pamoja na hayo alieleza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa Vyama Vya wafanyakazi katika kusaidia Waajiri na Serikali kwenye kuboresha mazingira ya kazi kwa ujumla.

“Serikali itaendelea kushirikiana nanyi katika kutekeleza shughuli mbalimbali kwa ajili ya kuiletea nchi yetu maendeleo,” alisema Mhagama

Pia, Waziri Mhagama alitumia fursa hiyo kukipongeza Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) pamoja na viongozi wa chama hicho kwa kukamilisha ujenzi wa jengo lao binafsi na kununua magari ambayo yatasaidia utekelezaji wa shughuli za chama.

“Hii ni ishara inayoonesha chama chenu kinaendelea kukua kiuchumi na yote hayao yanawezekana kutokana na nidhamu ya matumizi za fedha, uongozi bora na uwajibikaji,” alisema

Aidha, aliendelea kuwakumbusha Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi nchini kuzingatia falsafa ya serikali ya awamu ya tano ya kuendelea kujenga uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira ya utulivu na amani.

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Ndg. Tumaini Nyamhokya alisema kuwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa pamoja na majukumu makubwa waliyonayo wataendelea kuungana na Serikali katika kutatua kero za wananchi kwa kutoa huduma bora wakiongozwa na sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya kazi. Sambamba na hayo waliipongeza pia Serikali kwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.