Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Mhagama; Serikali Imedhamiria Kuwezesha Vijana kushiriki kilimo Biashara


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amesema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwezesha vijana kiuchumi kupitia kilimo biashara ili kuchochea ongezeko la ajira na kipato chao.

Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Baraza la Taifa la Biashara, kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji, tayari wilayani Kigoma wameanza kutekeleza Mradi unaolenga kuwezesha vijana kushiriki katika shughuli za uchumi kupitia mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali kwenye kilimo na ufugaji.

Akiongea katika ziara yake mkoani Kigoma wakati wa kukagua shughuli za utekelezaji za Baraza la Taifa la Biashara, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amefafanua kuwa Baraza la Taifa la Biashara kwa kushirikiana na Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji, wameanza utekekezaji wa mradi huo kwa kushirikiana na chuo cha Maendeleo Kihinga.

“Nitoe wito watendaji wa Halmashauri na ngazi ya mkoa wa Kigoma waendelee kuwaunga mkono vijana hawa wanao shiriki katika Mradi huu wa Kilimo Biashara, na nawataka mtambue haya yote yanafanyika kwa sababu ya jitihada zinazofanywa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, hivyo ufadhili wa Mradi huu kutoka Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji, unaunga jitihada zake za kuwezesha vijana” Amesisitiza Mhagama.

Naye Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (Masuala ya Majadiliano ya Sekta ya Umma na Binafsi), Andrew Mhina alibainisha kuwa katika kuhakikisha unawawezesha vijana kuwa na ujuzi wa Kilimo na ufugaji utakao wawezesha kujiajiri tayari wameanza ufadhili wa awali kwa kutoa kiasi cha shilingimilioni 53 ambazo zimetumika katika Ujenzi wa mabwawa ya samaki, ukarabati wa mabanda ya kufugia kuku na kuandaa shamba darasa.

Mradi wa Kuwezesha Vijana Kushiriki katika Kilimo Biashara wilayani Kigoma, Unaratibiwa na Baraza la Taifa la Biashara na ufadhiliwa na Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji chini ya wasimamizi na watekelezaji wa mradi huo amabao ni; Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia Manispaa ya Kigoma, Chuo cha Maendeleo Kihinga, Chuo cha Uvuvi Kigoma, Maradi wa LIC na Baraza la Biashara la Wilaya ya Kigoma.

Baraza la Taifa la Biashara lilianzishwa kwa Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2001 na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 39 la tarehe 28 Septemba 2001.Baraza la Taifa la Biashara ni jukwaa la majadiliano kati ya Sekta ya Ummana Sekta Binafsi. Lengo kuu la Baraza ni kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa njia ya majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.