Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

BAKWATA Yapongezwa Kuimarisha Amani, Umoja, Mshikamano Nchini


Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limepongezwa kwa kuimarisha amani, umoja na mshikamano nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusianao Mhe. Deus C Sangu wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi za Makao Makuu ya BAKWATA Januari 03, 2025 jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo imelenga kujitambulisha kwa viongozi wa Baraza hilo pamoja na kulitambulisha rasmi jukumu jipya la Mahusiano ambalo Ofisi ya Waziri Mkuu imekabidhiwa kuliratibu.

Mufti na Mwenyekiti wa BAKWATA, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally,

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Sangu amepongeza BAKWATA kwa mchango wake mkubwa katika kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Aidha, ameeleza kuwa Baraza hilo limekuwa nguzo muhimu ya maadili na mshikamano wa kijamii kwa kuhimiza mazungumzo ya amani, kuvumiliana na kuimarisha mahusiano mema baina ya waumini wa dini mbalimbali.

“Juhudi hizi zimechangia kwa kiasi kikubwa kudumisha utulivu na mshikamano wa kitaifa,” alisema Waziri Sangu.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kidini katika kushughulikia changamoto za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kikanda na kimataifa, hususan katika eneo la malezi bora na ujenzi wa jamii yenye maadili mema.

Sambamba na hayo, Waziri Sangu ameihakikishia BAKWATA kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, itaendelea kushirikiana kwa karibu na Baraza hilo pamoja na taasisi nyingine katika kuendeleza agenda ya amani, mshikamano na maendeleo jumuishi.

Kwa upande wake, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally amempongeza Rais Samia kwa kutambua umuhimu wa masuala ya Mahusiano na kuanzisha Wizara mahsusi inayoratibu eneo hilo.

Aidha, ameishukuru Serikali kwa kutambua na kuthamini mchango wa BAKWATA na kuahidi kuwa Baraza hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha umoja wa kitaifa, amani na mshikamano nchini.