Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ndalichako aanza kambi mikoa mitatu kutatua kero za Wastaafu


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof..Joyce Ndalichako ameanza kukutana na kuwasikiliza Wastaafu wa mifuko ya PSSSF na NSSF wanaopokea pensheni zao katika mkoa wa Dodoma.

Lengo la Mikutano hiyo ni kutatua changamoto za Wastaafu nchini zinazohusiana na ulipwaji wa mafao na Pensheni, ambapo ataanza na utaratibu huo katika mikoa ya Dodoma, Dar es salaam na Mwanza.

Akiongea na Wastaafu wanaopokea pensheni ndani ya mkoa wa Dodoma tarehe 20 Julai, 2022, Mhe. Ndalichako, amefafanua kuwa

“Haya ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye kila mara ametutaka viongozi tutoke na kuwasikiliza wananchi kero zao. Ni jukumu na ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za wananchi wakiwemo wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya jamii.”

Mhe. Ndalichako amefafanua kuwa amefanikiwa kumsikiliza mstaafu mmoja mmoja ambaye amefika kukutana naye, ambapo amebainisha kuwa baadhi ya Changamoto za wastaafu zinatokana na waajiri wao wa zamani kutotimiza wajibu wao, nyingine ni za kiutendaji ndani ya mifuko pamoja na uelewa mdogo juu ya masuala ya mafao na pensheni.

“Nimeona nitenge muda kusikiliza changamoto walizonazo wastaafu wa NSSF na PSSSF hivyo zile changamoto ambazo tunaweza kuzitatua papo kwa papo tunafanya hivyo na zile ambazo zinahitaji muda tunachukua vielelezo na kuzifanyi kazi”

Waziri Ndalichako amesema lengo la Serikali kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kuhakikisha wanatoa huduma kwa wastaafu bila usumbufu wowote na kuwahudumia kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazoongoza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Wakiongea kwa nyakati tofauti mamia ya wastaafu wanaopokea pensheni ndani ya mkoa wa Dodoma ambao wamefanikiwa kukutana na Mhe. Waziri Ndalichako, wameshukuru na kupongeza hatua hiyo ya kukutana nao kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua changamoto zao.

Aidha, wameongeza kuwa wanamshuru Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kumchagua Waziri Ndalichako ambaye ni msikivu, anayejali wazee, anayejali watumishi waliotumikia nchi hii kwa muda mrefu.