Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ndalichako: Serikali Kuendelea Kuwajali na Kuwathamini Wastaafu


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amewahakikishia wastaafu nchini kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutatua changamoto zinazowakabili wastaafu nchini.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo tarehe 28 Jijini Mwanza ikiwa ni muendelezo wake wa kukutana, kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wastaafu wa Mifuko ya PSSSF na NSSF, ambapo tayari alishakutana na wastaafu wa Jiji la Dodoma na Dar es Salaam.

Amesema Rais Samia anawajali na kuwathamini wastaafu wote nchini kutokana na mchango wao mkubwa walioutoa katika ujenzi wa uchumi wa nchi na ndio maana anataka kila mtumishi anayestaafu alipwe haki yake kwa mujibu wa Sheria.

“Nimeanza kukutana na wastaafu wetu kwani haya ni maelekezo ya Mhe. Rais Samia ambaye anawathamini sana wastaafu wetu hivyo nimekuja hapa Mwanza kusikiliza na kutatua kero zao,” alisema.

Waziri Ndalichako ametoa wito kwa waajiri wote nchini kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati kwani baadhi ya kero za wastaafu zinasababishwa na waajiri kutowasilisha michango kwa wakati.

Amebainisha kuwa kutokana na hali hiyo Wizara anayoisimamia itahakikisha inafanya kaguzi za mara kwa mara ili kuwabaini waajiri wote ambao hawawasilishi michango na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria.

“Waajiri wote wasimamie sheria bila shuruti kwa sababu sheria iko wazi mfanyakazi anakatwa asilimia kumi na mwajiri anaongeza asilimia kumi inapatikana asilimia 20 ambayo itawasilishwa kwenye mifuko,”

Amebainisha kuwa kwa upande wa watumishi wa umma Serikali imeona tatizo la baadhi ya waajiri hasa wa Halmashauri kutowasilisha michango ambapo kuanzia mwezi Julai mwaka 2022 tayari Serikali imechukua hatua kwa kukata moja kwa moja michango ya watumishi.

Waziri Ndalichako amesema baadhi ya changamoto za wastaafu ambazo amezibaini katika Jiji la Mwanza ni mapunjo ya mafao kwamba mstaafu na waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa NSSF na PSSSF jambo ambalo ni kinyume cha sheria.