News
Waziri Sangu Abainisha Mafanikio Makubwa Sekta ya Kinga ya Jamii
✅ Amesema Thamani ya Mifuko Yafikia Trilioni 24.20
Na: OWM (KAM) - Arusha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Clement Sangu, amebainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya kinga ya jamii nchini, ambapo thamani ya mifuko yote ya hifadhi ya jamii imeongezeka maradufu kutoka shilingi trilioni 10.43 mwaka 2020 hadi kufikia shilingi trilioni 24.20 mwezi Desemba 2025.
Mhe. Sangu amebainisha hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Kinga ya Jamii uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha wakati akimwakilisha Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Waziri sangu amesema kuwa ukuaji huo ni matokeo ya maboresho ya kisera na kisheria yaliyofanyika kuanzia mwaka 2018 kwa lengo la kukuza Maendeleo ya sekta ya kinga ya jamii.
“Ofisi ya Waziri Mkuu ina jukumu la kusimamia na kuratibu kinga ya jamii ambalo ni suala muhimu la kupambana na umaskini unaotokana na magonjwa, uzee, ulemavu na ajali kazini,” amesema
Vilevile, Waziri Sangu amefafanua zaidi kuwa idadi ya wanachama katika mfuko wa PSSSF na NSSF imeongezeka kwa asilimia 106 ndani ya miaka mitano, huku uwekezaji wa mifuko hiyo ukifikia shilingi trilioni 20.13 katika maeneo mbalimbali ikiwemo hati fungani za Serikali, miliki ardhi na hisa.
Kwa upande mwengine amesema, Mafanikio hayo yameenda sambamba na uimarishaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambao katika awamu ya pili pekee umeweza kunufaisha zaidi ya kaya milioni 1.37 zenye takribani watu milioni 5.5 kwa ruzuku ya zaidi ya shilingi trilioni 1.55. Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kutekeleza Mpango wa kunusuru kaya maskini ikiwa ni hatua muhimu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii na Dira 2050.
Kadhalika, Waziri Sangu amepongeza mfuko ya WCF kwa kuendelea kutoa fidia kwa wafanyakazi na mfuko wa NHIF kwa kuttoa huduma za matibabu kwa wananchi, ambapo NHIF sasa inahudumia wanachama na wategemezi zaidi ya milioni tano.
