Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Waziri Sangu: Rais Samia Awezesha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwa Himilivu


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa jitihada zake thabiti za kuendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha mifuko ya hifadhi ya jamii, pamoja na kuhakikisha utoaji wa pensheni unafanyika kwa wakati na kwa ufanisi.

Pongezi hizo zimetolewa Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Clement Sangu, wakati akitoa ufafanuzi wa hoja za wabunge waliochangia katika mjadala wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, uliokamilika tarehe 15 Aprili 2026.

Mheshimiwa Sangu amesema thamani ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) imeongezeka kutoka shilingi trilioni 4.36 hadi kufikia shilingi trilioni 10.3 sasa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeongezeka kutoka shilingi trilioni 5.74 hadi shilingi trilioni 12.96.

Katika hatua nyingine, Waziri Sangu ameeleza kuwa uimara wa mifuko hiyo umewezesha watumishi wa umma wanaostaafu kulipwa mafao yao ndani ya siku 25, huku kiwango cha chini cha pensheni kikiongezeka kutoka shilingi 100,000 hadi shilingi 250,000.

Akihitimisha mchango wake, Mheshimiwa Sangu aliwahakikishia wabunge kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano itaendelea kusimamia utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa ufanisi, ili kuleta manufaa kwa Watanzania katika sekta zote za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Mussa Azan Zungu, amewapongeza wabunge kwa kupitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kusisitiza umuhimu wa wizara na taasisi husika kusimamia utekelezaji wake ili kuchochea maendeleo ya wananchi.