News
Waziri Sangu: Serikali kuendelea kukuza ustawi wa Sekta ya Kazi na ushirikiano Kimataifa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu leo Juni 3, 2026 amefanya mazungumzo na Balozi Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Mhe. Dkt. Abdallah Possi na kueleza azma ya Serikali katika kukuza Ustawi wa Sekta ya Kazi na kuimarisha Ushirikiano wa Kimataifa.
Amesema hayo alipotembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Uswisi, akiwa katika ziara yake ya kikazi nchini humo inayolenga kushiriki Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) unaofanyika Jijini Geneva, Uswisi.
Katika mazungumzo yao na Balozi Possi wamejadili ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huo na manufaa yake makubwa kwa Taifa ikiwemo fursa za kuendeleza ushirikiano katika masuala ya kazi, kukuza ujuzi kwa nguvu kazi na kuongeza fursa za ajira.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Sangu alieleza dhamira ya Serikali katika kuendelea kuimarisha ustawi wa wafanyakazi, kukuza ajira zenye staha na kuhakikisha mazingira bora ya kazi. Pia, ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano na Shirika la Kazi Dunia pamoja na nchi wanachama wa ILO ili kujenga ushirikiano, kuvutia uwekezaji unaozalisha ajira na kuhakikisha Sera za kazi zinaendana na viwango vya kimataifa.
Sambamba na hilo, Waziri Sangu amepongeza ubalozi huo na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika masuala mbalimbali ili kuona fursa zilizopo Uswisi na kuwawezesha Watanzania kuzichangamkia fursa za kazi na ajira.
Akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa shughuli za ubalozi, Mhe. Dkt. Possi amepongeza ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huo wa 114 na kusisitiza kuwa Tanzania ina kila sababu ya kuendelea kushiriki katika mikutano hiyo ili kuwa na ustawi mzuri katika Sekta ya Kazi utakaowezesha nchi kupata na kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na Mikutano hiyo.
Wajumbe wengine walioshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Zuhura Yunus, Kamisha wa Kazi, Suzan Mkangwa, Kamishna wa Kazi Zanzibar, Rashid Khamis Othman, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, Mkurugenzi wa CMA, Usekelege Mpulla, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba Doran, Katibu Mkuu wa TUCTA, Hery Mkunda, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo, pamoja na Viongozi wengine kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi hiyo.


