Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Waziri Sangu: Taasisi za Dini ni Nguzo Muhimu ya Maendeleo Nchini


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema kuwa taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa jamii kwa kutoa huduma za kiroho, maadili na malezi bora, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa kuwa na maendeleo endelevu ya Taifa.

Aidha, amesema dhamira hiyo imedhihirishwa kwa vitendo na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikisha Taasisi za Dini katika masuala mbalimbali nchini.

Waziri Sangu amesema hayo leo Aprili 19, 2026 alipomwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika Harambee ya Ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Rulenge, Ngara. Harambee hiyo imefanyika katika ukumbi wa Kwatunza Beach Arena, Jijini Mwanza.

Akisoma hotuba hiyo, Waziri Sangu amesema Mheshimiwa Waziri Mkuu amewaomba Viongozi wa dini kuendelea kuwalea kiroho vijana ili waendelee kuwa na maadili, tabia njema, wazalendo na wenye kupenda Taifa lao, malezi bora kwa lengo la kuwa na jamii tulivu na yenye amani.

Vilevile, amehamasisha ushirikiano baina ya Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo Taasisi za Dini. Pia amepongeza taasisi za dini kwa namna zinavyoendelea kudumisha amani, mshikamao na utulivu pamoja na namna Viongozi wa dini wanavyojituma kwa bidii kuchapa kazi kwa ustawi wa Maendeleo ya Taifa.

Katika harambee hiyo, Mhe. Sangu amefanikiwa kuchangisha zaidi ya shilingi Milioni 114,982,000 ambapo katika pesa hiyo Waziri Mkuu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba amechangia Tsh. Milioni 30 taslimu.

“Tumekuja kushirikiana katika harambee hii ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya ibada Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Rulenge, Ngara ambayo itakuwa alama ya imani na mshikamano,” amesema Waziri Sangu

Naye, Muhashamu Baba Askofu wa Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi amesema kanisa hilo hadi kukamilika utagharimu shilingi bilioni 7.7 ambazo zitahusisha gharama za ujenzi na ununuzi wa thamani za kanisa.

Kwa upande mwengine, ameipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini nchini, akieleza kuwa ushirikiano huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ustawi wa jamii.